• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
Kazi kubwa kwa wanariadha ratiba mpya za IAAF na Diamond League zikitolewa

Kazi kubwa kwa wanariadha ratiba mpya za IAAF na Diamond League zikitolewa

Na CHRIS ADUNGO

MAKALA ya kwanza ya Riadha za Dunia za Continental Tour sasa yatafanyika jijini Nairobi mnamo Septemba 26, 2020.

Katika kalenda mpya msimu huu iliyotolewa na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF), fani za kushindaniwa katika kivumbi hicho pia zimepunguzwa kutoka 11 hadi tano pekee.

Haya yanajiri siku chache baada ya Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) kukiri kwamba litalazimika kuunga vikosi tofauti kwa minajili ya makala yajayo ya Riadha za Dunia na Jumuiya ya Madola nchini Amerika na Uingereza mtawalia.

Hii ni baada ya IAAF kuthibitisha kuwa mashindano hayo mawili ya haiba kubwa yataandaliwa kwa takriban kipindi kimoja; yaani mwishoni mwa 2021 na mwanzoni mwa 2022.

Awali, mbio za Continental Tour zilikuwa zimepangiwa kufungua rasmi kampeni za riadha msimu huu. Hata hivyo, ndizo zitakazokuwa sasa za mwisho kwenye kalenda mpya. Riadha za Gyulai Istavan Memorial ambazo awali ziliratibiwa kuandaliwa Julai 7 sasa zitakuwa za kwanza mnamo Agosti 20 mjini Szekesfehervar, Hungary.

Kivumbi cha Kamila Skolimowska Memorial ambacho pia kitajumuisha idadi kubwa ya Wakenya, kitaandaliwa mjini Silesia, Poland mnamo Septemba 6, siku mbili kabla ya mbio za Ostrava Golden Spike kufanyika nchini Czech.

Kivumbi cha Memorial Borisa Hanzekovica kilichokuwa kitifuliwe mjini Zagreb, Croatia mnamo Septemba 6, sasa kimeahirishwa hadi Septemba 15.

Kwingineko, vinara wa Diamond League wametoa ratiba mpya ya mbio hizo baada ya duru za Rabat, Zurich na London zilizokuwa ziandaliwe kati ya Aprili na Julai 2020 kufutiliwa mbali. Duru ya Monaco itakayofanyika Agosti, ndiyo itakayofungua sasa kampeni rasmi za Diamond League muhula huu.

“Fani nyingi zitapanguliwa na nyingine kufutiliwa mbali wakati ambapo waandalizi wanajitahidi kufanikisha kampeni za msimu huu ambazo zimevurugwa na corona,” ikasema taarifa yao.

Ina maana kwamba duru tatu za mbio za Diamond League zikitaandaliwa Agosti: Monaco (14), Gateshead Uingereza (16) na Stockholm (23).

Duru za Lausanne, Brussels, Paris, Shanghai na Roma zitaandaliwa Septemba huku za Naples, Eugene, Doha na Hong Kong zikihamishwa sasa hadi Oktoba 2020.

You can share this post!

Murkomen asema habanduki Jubilee

Wito serikali iweke vifaa muhimu kwa ajili ya walemavu...

adminleo