Mfumaji matata wa Harambee Stars atangaza mipango yake mara atakapostaafu soka
Na CHRIS ADUNGO
FOWADI wa Harambee Stars, Jesse Jackson Were, 31, ambaye ni mfungaji bora wa muda wote katika kikosi cha Zesco United nchini Zambia, ana mipango ya kujitosa katika biashara na kufungua akademia ya soka mara atakapostaafu kwenye ulingo wa kandanda.
Nyota huyo wa zamani wa Tusker aliyeanza kuvalia jezi za Zesco mnamo 2016 alikuwa akiyajibu baadhi ya maswali ya mashabiki wake kwenye mtandao wa Instagram.
“Baada ya kuangika rasmi daluga zangu, ningependa sana kuwekeza katika biashara na kufungua akademia ya soka kwa minajili ya chipukizi wanaojivunia utajiri mkubwa wa vipaji na talanta,” akasema.
Alisema kwamba Boniface Oluoch wa Gor Mahia ndiye kipa matata zaidi ambaye yeye amewahi kumkabili katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) na sogora wa zamani wa Harambee Stars, Jamal Mohammed ndiye kiungo bora zaidi ambaye yeye amewahi kucheza naye katika kikosi kimoja kwenye soka ya kimataifa.
Were pia alidokeza kwamba mshambuliaji Idriss Mbombo ambaye huchezea Nkana FC ambao ni watani wa tangu jadi wa Zesco, ndiye mchezaji ambaye yeye ‘anamtambua’ zaidi katika Ligi Kuu ya Zambia (ZSL).
“Mbombo ni mchezaji wa haiba kubwa ambaye huwa namfuatilia sana katika ZSL. Duniani, viungo ambao nilipenda sana kuwatazama uwanjani ni nyota wa zamani wa Barcelona, Xavi Hernandez na Andreas Iniesta. Kwa sasa navutiwa sana na kiwango cha ubora wa Kevin De Bruyne wa Manchester City,” akasema.
Alipoulizwa iwapo amewahi kuwazia uwezekano wa kubadilisha uraia wake na kuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Zambia almaarufu Chipolopolo, Were alisema hajawahi kuwa na azma hiyo licha ya kupuuzwa mara nyingi na makocha wa Harambee Stars katika michuano muhimu ya haiba.
Were alifunga bao la dakika za mwisho katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu ya ZSL dhidi ya Mufulira Wanderers mnamo 2017 na kuwanyanyulia Zesco United ufalme wa kipute hicho. Anasema hilo ndilo bao lake bora zaidi katika historia ya usogora.
Kasi uwanjani
Kulingana naye, beki wa zamani wa Gor Mahia, David ‘Calabar’ Owino ndiye mchezaji mwenye kasi zaidi katika kikosi cha Zesco United kwa sasa.
Kati ya wanasoka wote wa Harambee Stars kwa sasa, watano ambao Were anahisi kwamba wana ushawishi zaidi katika kikosi cha timu ya taifa ni kipa Arnold Origi, Victor Wanyama, Eric Johanna, Aboud Omar na Brian Mandela.
Mfumaji huyo anashikilia kwamba kati ya sifa ambazo mshambuliaji anastahili kuwa nazo ni udhibiti mzuri wa mpira, kuwepo katika pahala panapostahili kwa wakati ufaao na uwezo wa kutikisa nyavu kwa wepesi akitumia fursa chache anazopata ugani.
Were pia aliwaambia mashabiki wake kwamba mpinzani ‘mgumu’ zaidi ambayo yeye amewahi kukabiliana naye katika soka ya bara la Afrika ni kikosi cha Wydad Casablanca kutoka Morocco.
Mwanzoni mwa mwaka 2020 Were ambaye pia amewahi kucheza Mathare United na Kibera Black Stars baada ya kufanyiwa majaribio na wanabenki wa KCB, alitia saini mkataba mpya wa miaka miwili wa thamani ya Sh18 milioni kambini mwa Zesco United.
Hii ilikuwa baada ya kikosi cha Baroka FC kutoka Afrika Kusini kuanza kuyahemea maarifa ya Were.
Baroka kwa sasa wanatiwa makali na kocha wa zamani wa Gor Mahia, Dylan Kerr.
Hadi Ligi Kuu ya ZSL ilipoahirishwa kwa muda usiojulikana msimu huu kutokana na janga la corona, Were ambaye ni mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Upili ya Emusire, Kakamega alikuwa amefunga mabao 14.
Kufikia sasa, anajivunia magoli 94 kapuni mwake akivalia jezi za Zesco, idadi inayomfanya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa kikosi hicho.