Alikosea wapi?
BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano aliendelea na harakati zake za ‘kusafisha’ chama cha Jubilee baada ya kuwatema maseneta watano maalumu wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto.
Hatua zake, hasa zinazomlenga naibu wake zimeendelea kuibua maswali mengi miongoni mwa Wakenya, baadhi wakishangaa wawili hao walikosania wapi.
Uhusiano wao umeonekana kukumbwa na uhasama hivi kwamba, ni bayana Rais Kenyatta hatamuunga Dkt Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2017 Rais Kenyatta aliahidi wafuasi wa Jubilee kwamba, angetawala kwa miaka 10 na kumpisha Ruto atawale kwa miaka mingine 10 pia.
Uhasama wao unadhihirika katika matukio ya hivi punde ambapo Rais Kenyatta anawatimua wandani wa naibu wake wanaoshikilia nyadhifa za juu serikalini, bungeni na katika mashirika ya serikali.
Jumatano, maseneta hao walifurushwa kwa kususia mkutano ulioongozwa na Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi Jumatatu.
Walioandikiwa barua za kufurushwa ni pamoja na Millicent Omanga, Falhada Dekow Iman, Naomi Jillo Waqo, Victor Prengei na Mary Seneta.
Watano hao ni washirika wa Naibu Rais William Ruto na ndiye alishawishi uteuzi wao.
Kulingana na taarifa fupi iliyotolewa na Katibu Mkuu Raphael Tuju mnamo Jumatano, watano hao walifukuzwa kwa mienendo mibaya na kukosa heshima kwa uongozi wa chama.
“Walipokea mwaliko wa mkutano lakini hawakujali hata kuomba radhi kwa kutohudhuria,” akasema Tuju.
Hata hivyo, wandani wa Dkt Ruto katika Seneti wameshikilia kuwa hawakualikwa katika mkutano huo.
Ni katika kikao hicho kilichohudhuriwa na maseneta 20 kati ya 35 ambapo maseneta Kipchumba Murkomen na Susan Kihika, waliovuliwa nyadhifa za kiongozi wa wengi na kiranja wa wengi, mtawalia.
Wadadisi wa siasa wanasema Rais Kenyatta alikosa imani na Dkt Ruto kwa kuonekana kukaidi maagizo yake na mwelekeo alioutaka kiongozi wa nchi.
“Ruto alikosea kwa kumdharau Rais na hivyo kufanya kiongozi wa nchi na wandani wake kukosa imani naye. Hisia zao wandani wa Rais ni kuwa, Ruto ni hatari na hafai kuwa Rais na wakaanza mipango ya kumkata kucha polepole. Tunachoshuhudia sasa ni kilele cha njama iliyoanza kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017,” asema Bw David Gatura mdadisi wa masuala ya siasa.
Anasema Rais Kenyatta amekuwa akimvumilia Dkt Ruto lakini akazidisha kiburi.
“Hakuna kiongozi wa nchi anayeweza kufurahishwa na naibu anayejipiga kifua kuwa ana umaarufu kumliko. Hivyo ndivyo Dkt Ruto alivyofanya kwa kuendeleza siasa na kuvamia ngome yake ya Mlima Kenya. Ilikuwa ni kumhujumu Rais na hii ni sawa na mapinduzi,” alisema Bw Gatura.
Kulingana na naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee, Bw David Murathe, wandani wa Rais Kenyatta walikosa imani na Dkt Ruto kwa sababu ya tabia yake.
Bw Murathe amenukuliwa mara kadhaa akisema Dkt Ruto ni mkaidi na hawezi kulinda maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya akiwa Rais.
“Ikiwa anamkaidi Rais akiwa naibu wake, itakuwaje akiwa mamlakani?” Bw Murathe amekuwa akiuliza.
Mbunge mmoja wa Jubilee ambaye hakutaka tutaje jina lake alisema kiburi cha Dkt Ruto kilimfanya aamrishe baadhi ya mawaziri.
“Haya yalikuwa makosa makubwa na Rais alikasirika. Alianza kushawishi wabunge kumuasi Rais Kenyatta hasa katika vita dhidi ya ufisadi na Mpango wa Maridhiano (BBI). Licha ya kushauriwa na Rais mara kwa mara alimpuuza na kutaka kuonekana kuwa kiongozi wa chama akijigamba alivyo na idadi kubwa ya wabunge. Nafikiri kulikuwa na njama dhidi ya Rais ambayo ilitibuliwa na handisheki,” alisema mbunge huyo.
Msimamo wa Dkt Ruto kuhusu BBI na vita dhidi ya ufisadi, uligawanya chama cha Jubilee katika makundi ya ‘Tangatanga’ la wabunge wanaomuunga mkono na ‘Kieleweke’ linalomuunga Rais Kenyatta.
Baadhi ya wadadisi wanahisi Rais Kenyatta na Dkt Ruto walitofautiana kisera katika kipindi cha pili uongozini.
“Rais alitaka kuacha kumbukumbu na mwingine alitaka kujiandaa kwa uchaguzi wa 2022 na wakajipata njia panda,” mdadisi wa siasa Geff Kamwanah anaeleza.