Habari

COVID-19: WHO yawataka watu waishi kwa tahadhari kuu jinsi wafanyavyo kudhibiti Ukimwi

May 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

GENEVA, Uswisi

VIRUSI vya corona ambavyo husababisha ugonjwa wa Covid-19 huenda vikasalia sugu kama virusi vya HIV, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limesema.

Hii ni licha ya juhudi zinazoendeshwa za kudhibiti kusambaa kwake.

“Ni muhimu kuweka ukweli huu katika meza: virusi hivyo vitageuka kuwa sugu katika jamii zetu, na virusi hivyo havitatokomezwa haraka,” mtaalamu wa WHO anayesimamia milipuko ya magonjwa Mike Ryan akasema katika taarifa kupitia mitandaoni.

Akaongeza: “Nadhani ni muhimu kuzingatia ukweli na sidhani kama yeyote anaweza kubashiri ni lini ugonjwa huu utaisha.”

Amesema kufikia sasa WHO haiwezi ikatoa ahadi kuhusu janga hili ya ni lini litadhibitiwa.

Hata hivyo, amesema kuwa juhudi zinaendelezwa za kusaka chanjo dhidi ya ugonjwa huu lakini “ni kibarua kigumu mno.”

Zaidi ya chanjo 100 zinatayarishwa huku majaribio kadha yakifanywa.

Lakini wataalamu bado wanakiri kuwa wanakabiliwa na kibarua kigumu zaidi kupata chanjo inayoweza kudhibiti virusi vya corona.

Ryan amesema chanjo nazo zina changamoto zao, akitoa mfano wa chanjo nzuri dhidi ya magonjwa mengine kama ukambi, lakini ambao haujatokomezwa kabisa kufikia sasa.

Ryan amesema mikakati madhubuti ya kudhibiti virusi vya corona inahitajika ili kupunguza makali na athari zake ambazo ni za kiwango cha juu katika ngazi za kitaifa, kikanda na ulimwenguni kote.

Wakati huu Serikali za Mataifa kadhaa ulimwenguni zinatafakari haja ya kufungua chumi zao huku zikiendelea kutekeleza mipango ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Kufikia sasa ugonjwa wa Covid-19 umewapata takriban watu 4.3 milioni na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 291,000 kote duniani.

Jumatano, Muungano wa Ulaya (EU) ulishinikiza mataifa wanachama kufungua mipaka yao ambayo imefungwa kwa sababu ya janga la corona.

Ulisema sekta ya utalii inaweza kufunguliwa msimu huu wa joto huku masharti ya usalama yakizingatiwa.

Lakini wataalamu wa afya wanashauri kuwa uangalifu mkubwa unafaa kuzingatiwa kuzuia kutokea kwa milipuko mipya ya Covid-19.

Ryan amesema kufunguliwa kwa mipaka ya ardhi hakuwezi kusababisha hatari kubwa sawa na kufunguliwa kwa safari za angani.