COVID-19: Ni masharti makali kwa wanasoka mechi za ligi zikirejea
Na CHRIS ADUNGO
“KUTOTEMA mate” ni mojawapo ya mapendekezo ambayo vinara wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) wamesisitiza katika mwongozo kwa wanasoka wa kipute hicho kinachotarajiwa kurejelewa wikendi ya Mei 16, 2020.
Waendeshaji wa Bundesliga (DFL) wamepania kutalii mbinu zote zitakazowawezesha wadau wa soka kufanikisha mipango ya kukamilisha kampeni za msimu huu licha ya kwamba janga la virusi vya homa kali ya corona halijadhibitiwa vilivyo.
Mbali na wachezaji kutotema mate, taratibu nyinginezo ambazo zimetolewa ni wanasoka kutokabiliana kwa karibu sana wakati wa mechi na viwanja kusalia vitupu kwa kukosa mahudhurio ya mashabiki.
“Tutahitaji kiwango kikubwa cha nidhamu ili kuyafikia maazimio yetu katika msimu huu wa 2019-20 kwenye soka ya Bundesliga,” ikasema sehemu ya taarifa ya DFL.
Utaratibu
Siku ya mechi, maafisa wa afya wa vikosi husika watahitajika kuwasilisha fomu kwa vinara wa DFL kuthibitisha kuwa wanasoka wote wamefanyiwa vipimo vya afya kubaini iwapo wana virusi vya corona au la.
Iwapo ripoti hiyo haitawasilishwa kufikia saa nne na nusu asubuhi, basi pendekezo la kufutiliwa mbali kwa mechi litatolewa.
Usafiri
Vikosi vya kigeni vitatakiwa kusafiri kwa kutumia idadi kubwa iwezekanavyo ya mabasi ili kuhakikisha kwamba umbali wa mita moja na nusu kati ya wachezaji unadumishwa.
Wanasoka wanaochezea nyumbani wanastahili kuwasili ugani kwa magari yao binafsi, kila mmoja akijiendesha.
Watu uwanjani
Viwanja vimegawanywa katika zoni tatu: sehemu ya ndani (pa mechi kuchezewa, wanasoka kuingilia na pa kubadilishia sare); sehemu ya mashabiki kukalia na ile inayozingira uwanja kwa nje.
Ni wajibu wa klabu inayochezea nyumbani kuhakikisha kwamba kila sehemu haitakuwa na zaidi ya watu 100 kwa wakati mmoja.
Sehemu ya ndani itakuwa ya wachezaji pekee, wanasoka wa akiba, maafisa 10 wa vikosi, ma-ballboy wanne watakaovalia glavu na barakoa, wapiga-picha watatu, maafisa watatu wa kutoa huduma za kwanza za afya, waelekezi wanne na wataalamu 15 wakaohusika katika upeperushaji wa mechi, kurejelewa kwa video na ukusanyaji wa data.
Kikosi cha nyumbani kitakuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba hakuna mashabiki katika zoni zote tatu za uwanja.
Mbali na wataalamu wa masuala ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli, sehemu ya mashabiki itakuwa pia na wafanyakazi watakaoruhusiwa kufanya usafi wa uwanja kabla ya mechi, mwisho wa mechi au wakati wa mapumziko.
Vyumba
Kila uwanja utakuwa na vyumba vingi iwezekanavyo vya wachezaji kutumia kubadilishia nguo katika juhudi za kuhakikisha kwamba hawatangamani kwa karibu. Vyumba hivi vitanyunyiziwa dawa za kuua virusi mara kwa mara.
Kuingia
Timu zitaingia uwanjani kwa nyakati tofauti na kwa kipindi tofauti na maafisa au waamuzi wa mchuano.
Hapatakuwepo na watoto watakaondamana na wachezaji wanapoingia ugani kama ilivyo desturi.
Manahodha wa timu pinzani hawatasalimiana mkono kwa mkono wala kuwasalimu pia maafisa wa mechi wakati wa kurushwa kwa sarafu.
Benchi
Wachezaji wa akiba watakalia umbali wa viti viwili au vitatu kwenye benchi. Wote watatakiwa kuvalia barakoa. Ni kocha pekee atakayeruhusiwa kutoa barakoa yake wakati wa kutoa maagizo kwa wachezaji mradi tu adumishe umbali wa mita moja na nusu kutoka kwa wanaomzingira.
Wachezaji watakaokuwa wakipasha misuli joto kabla ya kuleta nguvu mpya ugani hawatakuwa na ulazima wa kuvalia barakoa.
Kusherehekea
Hakuna kusherehekea bao kwa pamoja, kupigana pambaja wala wachezaji kusalimiana mkono kwa mkono. Kugusanisha kumbo au miguu kutakubaliwa. Hakuna kusalimiana kwa wachezaji wanaobadilishana nafasi ugani. Hakuna chupa za maji zitakazotolewa kwa wanasoka ambao pia watatakiwa kujizuia kabisa kutema mate uwanjani.
Baada ya mechi
Mikutano kati ya makocha na wachezaji kwa lengo la kutathmini mechi ilivyokuwa itaandaliwa mitandaoni.
Mahojiano mafupi na machache zaidi ndiyo yatakayoruhusiwa uwanjani baada ya mechi japo wahusika wote watatakiwa kuzingatia kanuni zilizopo za afya.