Habari

Majaji watatu washinda kesi ya kususia kazi

May 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MAJAJI watatu wa Mahakama ya Juu walishinda kesi waliyoshtakiwa mlalamishi akitaka wafukuzwe kazi akidai walikuwa wamesusia kazi.

Watatu hao Jaji Mohammed Ibrahim, Jaji Jackton Ojwang na Jaji Njoki Ndung’u walikuwa wameshtakiwa na aliyekuwa afisa mkuu wa chama cha wanasheria nchini (LSK) Apollo Mboya.

Akitupilia mbali kesi hiyo Jaji Weldon Korir alisema tume ya kuajiri watumishi wa idara ya mahakama (JSC) haina mamlaka kisheria kuwaadhibu majaji wa mahakama kuu.

Jaji Korir alisema majaji hao watatu hawakukaidi sheria yoyote kuwezesha wachukuliwe hatua ya kinidhamu.

Mboya alikuwa ameomba JSC iwatimue kazini kwa vile walikuwa wamesusia kazi wakilalama kuhusu sheria ya kustaafu.

Watatu hao walikuwa wameandikia JSC kuhusu agizo la Msajili mkuu wa Idara ya Mahakama Anne Amadi kuwaandikia barua aliyekuwa naibu wa Jaji Mkuu Kalpana Rawal na Jaji wa Mahakama kuu Philip Tunoi.

Katika barua hiyo Amadi alikuwa amewataka DCJ Rawal na Tunoi wasiwe wanahudumu kwa vile wamehitimu umri wa kustaafu wa miaka 70.

Majaji hao wawili walikuwa wamepinga agizo la JSC wastaafu wakisema walipoajiriwa walielezwa watastaafu wakihitimu umri wa miaka 74.

JSC iliwaandikia barua ya kuwaadhibu.

Jaji Korir alisema JSC ilikaidi Katiba ilipojitwika jukumu la kuwakemea majaji Ibrahim, Ojwang na Ndung’u.

Jaji Korir alifutilia mbali uamuzi huo wa JSC wa kuwakemea majaji hao mnamo 2016.

Jaji Ndung’u alikuwa amewasilisha ombi katika mahakama kuu kupinga uamuzi wa JSC wa kuwakejeli na kuwashutumu kwa kususia kazi.

Mboya alikuwa amewasilisha kesi katika JSC akiomba watatu hao watimuliwe kazini kwa kukaidi sheria na Katiba akidai walivuruga utendakazi wa Mahakama ya Juu.

Agizo la majaji wastaafu wakiwa na umri wa miaka 70 lilikuwa limeidhinishwa na aliyekuwa Jaji Mkuu Dkt Willy Mutunga.

Jaji Korir alisema kesi ya Mboya ilikuwa haina mashiko kisheria kuomba majaji hao wa mahakama ya juu watimuliwe kazi.

Akijitetea, Jaji Ndung’u alikuwa amesema JSC ilikosea sheria kuruhusu wahojiwe kutokana na msimamo.

Mboya alikuwa amesema kususia kazi kwa watatu hao kulisababisha upungufu wa majaji na kesi zilikuwa zimelundikana.