• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MAZOEZI: Baadhi ya wakazi wa mitaa iliyoko Thika Road wakimbia mbio za masafa kupunguza unene

MAZOEZI: Baadhi ya wakazi wa mitaa iliyoko Thika Road wakimbia mbio za masafa kupunguza unene

Na SAMMY WAWERU

KWA kawaida barabara ya Thika Superhighway, inayounganisha mji wa Thika na jiji la Nairobi, huwa na shughuli chungu nzima za usafiri na uchukuzi.

Pembezoni, imepakana na mitaa kadhaa ikiwamo Roysambu – Kasarani, Zimmerman, Githurai, Ruiru, miongoni mwa mingineyo.

Mchana shughuli za kibiashara huwa zimenoga katika mitaa hiyo, kafyu ya kati ya saa moja jioni hadi saa kumi na moja asubuhi, kila siku, inayoendelea ili kusaidia kudhibiti usambaaji wa Covid-19 ikizuia kukuza uchumi saa 24 kwa siku.

Hata hivyo, saa za amri hiyo zinapokamilika alfajiri na mapema, kati ya saa kumi na moja na dakika kumi hivi hadi saa moja asubuhi, kati ya mtaa wa Roysambu na Githurai, kandokando mwa Thika Superhighway hugeuzwa uga. Si uga wa soka au raga, ila uga wa ‘mazoezi na riadha’.

Ni mwendo wa saa kumi na moja na dakika ishirini hivi, Taifa Leo inafanya ziara ya kipekee eneo hilo.

Watu kadhaa, ambao ni wakazi wa mitaa jirani, waliovalia mavazi ya kispoti na njumu, wanashiriki riadha.

Wanakimbia kwa makundi, na baada ya kila dakika tano au kumi, wananyoosha viungo vya mwili. Muda unavyozidi kuyoyoma, idadi inaendelea kuongezeka.

Saa kumi na moja na dakika arubaini, watu wanaokadiriwa kuwa 30, wakijumuisha watoto, wanakuwa wenyeji wa mazingira hayo.

Kibwagizo kinakuwa ‘riadha na mazoezi’, wengine wakikariri dakika wanazonyoosha viungo vya mwili; miguu, mikono na shingo.

Vivian Sirima, mmoja wa ‘wanariadha hao’ na ambaye ni mkazi wa Zimmerman, anasema janga la Covid – 19 limesababisha awe na muda mrefu wa ziada.

“Ninafanya kazi ya ususi, na sekta hiyo imeathirika kwa kiasi kikuu. Ninaifanya kupitia oda, hivyo basi nina muda mwingi wa kupumzika. Ninakula na kunywa, na tangu athari za corona zitulazimishe kusalia nyumbani ninaendelea kuongeza unene na uzani. Nisingetaka kuibuka na shida za kiafya, riadha na mazoezi ya alfajiri na mapema, yamenisaidia kuimarisha mwili na viungo,” Vivian ambaye pia ni mama wa watoto wanne anafafanua.

Itimiapo mwendo wa saa kumi na mbili hadi saa kumi na mbili na nusu, idadi inaongeza mara dufu.

Kivuko cha daraja kilicho kati ya Roysambu na Githurai, kinasheheni shughuli za mazoezi, wakitumia vyuma vya kivuko hicho kunyoosha viungo vya mikono na miguu.

Washirika ni jinsia ya kiume na kike, ingawa watoto ni wachache walioandamana na wazazi wao.

Ni shughuli inayoendelea kwa muda wa takriban dakika kumi na tano, wengine wakiendelea kutimka mbio na kurejea kivukoni.

Nancy Wanjiru, kutoka Marurui, Nairobi, hata ingawa anauguza majeraha ya mazoezi, anasema anayashiriki kwa sababu ya kuwa na muda mrefu nyumbani.

“Nina muda mwingi wa ziada na ninashinda mchana bila kufanya chochote. Ili kuondoa machovu ya kutofanya kazi (boredom), ninalazimika kushiriki riadha na mazoezi,” Nancy ambaye ni mwalimu asema, akifichua kwamba huandamana na bintiye mwenye umri wa miaka tisa.

“Yuko gredi ya tano na huu ni mwezi wa pili wanafunzi kote nchini wakiwa nyumbani. Shuleni hufanya mazoezi ili kuwapevusha. Anafurahia kushiriki mazoezi haya,” mama huyo akasema kwenye mahojiano.

Ugonjwa wa Covid-19 ni janga la kimataifa lililoathiri sekta mbalimbali, ikiwamo ya elimu, biashara, utalii na uchumi wa mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Ili kuzuia maambukizi ya corona, Rais Uhuru Kenyatta Machi 2020 aliagiza shule na taasisi zote za masomo nchini kufungwa mara moja.

Shule zilipaswa kufunguliwa mapema Aprili, ila athari za corona zililazimu muda wa likizo kuongezwa hadi Juni, Waziri wa Elimu Prof George Magoha akiahidi ratiba ya mitihani ya kitaifa haitaathirika.

Itimiapo mwendo wa saa moja na nusu, wanaoshiriki mazoezi hayo wanaanza kurejea makwao. Wataalamu wa masuala ya afya wanasema mazoezi yanapaswa kuwa ratiba ya kila wakati, ili kunyoosha viungo vya mwili na vilevile kujiepusha dhidi ya magonjwa yanayohusishwa na afya.

“Mbali na kufanya viungo kuwa imara, mazoezi hupunguza uzito wa mwili na kiwango cha mafuta mwilini yanayotia mtu katika hatari ya kuugua ugonjwa wa pumu, shinikizo la juu la damu, kisukari, miongoni mwa mengine,” ashauri Andrew Kunyu, muuguzi na mtaalamu wa masuala ya siha.

You can share this post!

MABADILIKO: Mike Tyson mkulima hodari wa bangi baada ya...

COVID-19: Rais Kenyatta atarajiwa kutangaza hatima ya kafyu...

adminleo