• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
BURUDANI: Alikawia kujitosa kwa muziki kwa kudhania ulikuwa wa ‘watu wenye pesa’

BURUDANI: Alikawia kujitosa kwa muziki kwa kudhania ulikuwa wa ‘watu wenye pesa’

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

DIANA Mwamburi almaarufu Dianah Dinah hakufikiria siku moja ataweza kutimiza ndoto yake ya kuwa mwimbaji.

Fikra alizokuwa nazo Dianah ni kuwa mwimbaji ni lazima mtu awe tajiri na hilo ndilo lilomchelewesha yeye kuanza kujitosa katika fani hiyo ambayo ilikuwa moyoni mwake tangu utotoni alipokuwa akienda kanisani huku akivutiwa na kuwasikia waimbaji wa Injili.

“Ningekuwa mbali katika fani hii kama ningeanza kuimba kitambo kwani nilipenda kuwa mwimbaji wa nyimbo za Injili lakini uoga wangu mkubwa ulikuwa nilifikiria kuwa ni lazima uwe tajiri ndipo uwe mwimbaji,” akasema msanii huyo.

Ni lipi hasa lilomwezesha akaanza kuimba baada ya kupoteza muda mrefu?

Dianah anasema ni wakati mwimbaji John Issa aliimba wimbo wake wa ‘Usichoke’ akimshirikisha msanii mwenzake Anastacia Mukabwa na kumshirikisha kama mchezaji katika video yake ya kibao chake hicho, ndipo alipoondoa fikra alizokuwa nazo awali.

“Nilitiwa moyo na Issa pamoja na watu wengine waliofahamu kuwa nimekuwa nikitunga nyimbo zilizotumiwa na wanafunzi wa shule za upili ambazo nyingi ziliibuka za shindi, na ndipo nilipoanza kuimba nyimbo ambazo mashairi nayatunga mimi mwenyewe,” akasema.

Anamshukuru sana Issa kwa kumsaidia kutoa kibao chake cha kwanza na kumpa moyo kuwa aweza kuwa miongoni mwa waimbaji wazuri wa Injili sio hapa Kenya pekee bali Afrika Mashariki na Afrika.

Mwimbaji Diana Mwamburi ‘Dianah Dinah’. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Dianah, msanii anayependa kuongea kwa utaratibu na mcheshi, alifanikiwa kutoa kibao chake cha kwanza cha ‘Salama’ Oktoba 2019 ambacho kiliitikiwa vizuri na kumpa moyo mkubwa wa kuendeleza juhudi zake za kutaka kuwa mwimbaji wa kutambulika.

“Kuzindua kwa wimbo huo kulinipa moyo mkubwa wa kuhakikisha nafanya bidii kutoa nyimbo nyingine ambazo tayari ninazitia mahadhi kwani mashairi ninayo tele!” akasema Dianah.

Wimbo wake wa pili ‘Umenitengeneza’ aliuzindua hivi hazijapita siku nyingi na ana matumaini makubwa utavutia wasikilizaji wengi zaidi kwenye YouTube, Facebook na Instagram.

“Nashukuru nimekuwa maarufu kwa kipindi kifupi na nitajitahidi nitambulike kimataifa,” akasema.

Anasema alishawishiwa sana kujitosa kuimba nyimbo za karne mpya lakini kwake anasema moyo wake wote uko kwa kumtumikia Bwana.

“Nimeona kuna umuhimu wa kuimba nyimbo ambazo zitawafaidisha watu kujua umuhimu wa kufuata mafunzo ya dini,” anasema Dianah.

Msanii huyo anasema hakupendelea kuimba nyimbo za kisasa – maudhui ya anasa za kidunia – kama alivyoshawishiwa na marafiki zake kwa sababu alitambua huenda angeimba nyimbo ambazo ni kinyume na maadili ya Ukristo.

Udogoni alikuwa hodari zaidi kutunga mashairi ambayo yalikuwa yakitumika na baadhi ya shule za msingi na sekondari ambazo zilikuwa zikishiriki kwenye mashindano ya Tamasha za Muziki.

“Pia mashairi yangu yalikuwa yakitumika kwenye harusi na sherehe mbalimbali zikiwemo zile za mikutano ya siasa na kwenye harambee za kuchangia miradi ya maendeleo,” akasema Dianah ambaye anatumia mtindo wa chakacha katika nyimbo zake sababu anaamini ndio mtindo wa utamaduni wa Pwani.

Hapa nchini Kenya, anapenda kusikiliza nyimbo za kina Sarah K, Wilberforce na Anastacia nako huko Tanzania, yeye ni shabiki wa Rose Muhando kwa sababu ya mdundo wa nyimbo zake anaosema unachangamsha.

Anapanga mikakati ya kwenda jijini Dar es Salaam, Tanzania ambapo anatarajia kutafuta fursa ya kukutana na waimbaji wa Injili kwa minajili ya kupata japo kitu kidogo cha kuendeleza kipaji cha uimbaji wake.

Amesema waimbaji wa Injili wanazidi kuwa wengi kwa sababu wameona faida ya kueneza neno la Mungu.

“Sisi waimbaji wa Injili hatutegemei sana kipato bali zaidi ni kueneza mawaidha ya kuwasihi watu wafuate nyendo anazopenda Mungu,” akasema Dianah.

Amewaomba waimbaji wa nyimbo za kisasa wanaoinukia wajitahidi kuinua vipaji vyao kwa kuimba nyimbo ambazo zitakuwa zenye lugha nzuri na wajiepushe kutumia lugha ambazo zinaweza kuwapoteza vijana kujitumbukiza kwenye mashimo ya dhambi.

Dianah anawaambia mashabiki wake wasubiri kwa hamu nyimbo zake tatu zitakazofuatana mwaka huu wa 2020 za ‘Asante Yesu’, ‘Namtangaza Yesu’ na ‘Sela Bwana’ aliouimba kwa Kitaita kumaanisha ‘Tawala Yesu’.

You can share this post!

Safari Rally yasogezwa 2021 kwa sababu ya corona

Froome arejelea mazoezi huku akitazamiwa kuvunja ndoa kati...

adminleo