Michezo

Froome arejelea mazoezi huku akitazamiwa kuvunja ndoa kati yake na kikosi cha Ineos

May 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

CHRIS FROOME ambaye ni bingwa mara nne wa mashindano ya uendeshaji baiskeli ya Tour de France, amerejelea mazoezi ya nje huku tetesi za kubanduka kwake kambini mwa Ineos zikishika kasi.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 alianza mazoezi kwenye barabara za jiji la Monaco, Ufaransa mnamo Mei 15, 2020 baada ya kanuni za afya kuhusiana na janga la corona ‘kulegezwa kiasi’ kwa baadhi ya wanamichezo wanaoshiriki mazoezi kivyao katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe nchini Ufaransa, Froome ambaye ni mzawa wa Uingereza, anaviziwa na vikosi vingi maarufu vya bara Ulaya ambavyo vipo radhi kumshawishi wa ofa nono ili aagane na Ineos msimu huu.

Kwa upande wao, Ineos wameshikilia kwamba Froome angali na mkataba nao na aliwahi kuhakikishia usimamizi kwamba angekatiza uhusiano wake na Ineos mwishoni mwa 2021.

Ineos wanajivunia waendeshaji baiskeli mahiri zaidi walio na uwezo wa kuteuliwa kuwa ‘viongozi wa kikosi’ katika mapambano ya Tour de France. Miongoni mwao ni chipukizi Egan Bernal, 21, aliyetawazwa mwendeshaji bora zaidi wa baiskeli muhula jana.

Kujiunga na kikosi kingine kitakachompa Froome uhakika wa kuwa kiongozi wa kikosi kutakuwa nafuu zaidi kwa Mwingereza huyo badala ya kupigania ubabe na makinda wengi kambini mwa Ineos.

Majuzi, Bernal alisema: “Siwezi kabisa kutupa nafasi maridhawa ya kujinyanyulia mataji ya haiba katika kampeni za Tour de France nikiwa kiongozi wa kikosi na kumwachia mchezaji mwingine fursa hizo adimu. Sidhani hilo litawezekana nikiwa hapa Ineos.”

Froome anajivunia kutawazwa bingwa wa France de Tour ambayo ni miongoni mwa mashindano ya haiba kubwa zaidi katika ulimwengu wa uendeshaji baiskeli mnamo 2013, 2015, 2016 na 2017. Alipoteza ufalme huo mnamo 2018 baada ya kuzidiwa maarifa na Geraint Thomas wa Ineos.

Froome amewahi kusisitiza kwamba anapania kutia kapuni mataji zaidi katika makala yajayo ya Tour de France kabla ya kustaafu. Hata hivyo, alikosa fursa ya kunogesha kipute hicho msimu jana baada ya kuhusika katika ajali iliyomwacha na shingo, mkono, paja na mbavu zilizovunjika.

“Ndoto yangu ni kustaafu nikijivunia idadi kubwa zaidi ya mataji ya Tour de France kuliko mwendeshaji baiskeli mwingine yeyote katika historia ya mashindano hayo,” akasema Froome katika mahojiano yake na gazeti la L’Equipe.