• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Kenyatta Primary ya mjini Thika yafanyiwa ukarabati

Kenyatta Primary ya mjini Thika yafanyiwa ukarabati

Na LAWRENCE ONGARO

WALIMU na wanafunzi wa shule ya Kenyatta Primary mjini Thika wana sababu ya kutabasamu baada ya shule hiyo kufanyiwa ukarabati.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema Ijumaa kuna haja ya kuleta mabadiliko katika shule za msingi katika eneobunge lake ili wanafunzi wawe na mazingira mazuri ya kuchangia kutia bidii masomoni.

“Lengo langu kwa sasa ni kukarabati shule zote za Thika ili kuwe na mabadiliko ya kimazingira katika shule za msingi,” alisema Bw Wainaina.

Alisema wakati huu wanafunzi wako nyumbani kuna nafasi nzuri ya kurekebisha madarasa yao ili wakirejea tena wapate mabadiliko shuleni.

“Iwapo wanafunzi na waliimu wao watakuwa katika mazingira yafaayo, bila shaka hata hali ya masomo itabadilika pakubwa,” alisema Bw Wainaina.

Shule ya msingi ya Kenyatta iliyoko mtaa wa Makongeni, Thika ina wanafunzi wapatao 1,700.

Anasema kwa zaidi ya miaka miwili shule 30 zimefanyiwa ukarabati na kuwa katika hali ya kisasa.

Lengo lake la kukarabati shule zote za msingi ni kuona ya kwamba hali ya mazingira ya elimu inaboreshwa.

Athena

Alisema shule ya msingi ya Athena ilifanyiwa ukarabati mwaka wa 2019, ambapo kabla ya hapo madarasa yalikuwa katika hali mbovu ajabu.

“Wanafunzi wengi waliketi kwenye mawe kama dawati. Madirisha pia yalikosa kwenye madarasa hayo, huku walimu wakikosa viti vya kukalia ofisini,” alisema Bw Wainaina.

Alisema fedha za Maendeleo za NG-CDF ndizo zimetumika katika ukarabati huo wote wa shule hizo.

Zingine zilizofanyiwa ukarabati ni General Kago na Kisiwa.

Alitoa mwiti kwa wazazi wawe mstari wa mbele kuwashauri wana wao ambao wako katika ‘likizo ya lazima’ kutokana na Covid-19; maradhi yanayoyumbisha dunia tangu Desemba 2019.

“Kila mzazi ana jukumu kuona ya kwamba mtoto wake anafuata maagizo ya serikali ya kukaa nyumbani bila kuzurura ovyo. Huu ni wakati wa kujihusisha na Kazi za shule,” alisema mbunge hiyo.

Alisema iwapo kila mmoja atafuata maagizo ya serikali ya kudumisha usafi kwa kunawa mikono, kuvalia barakoa, na kuweka nafasi ya mita moja au zaidi baina ya mtu na mwenzake, bila shaka “tutaweza kupunguza homa ya corona ambayo tayari imekita hapa nchini kwetu.”

You can share this post!

Ligi kuu ya hoki kurejelewa mwezi mmoja baada ya Covid-19...

Je, ni upi mtazamo wako kuhusu uchoraji chale...

adminleo