Habari

'Hatuna ubaya'

May 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JUSTUS OCHIENG

WABUNGE na maseneta wanaomuunga mkono Naibu Rais, Dkt William Ruto wameingiwa na baridi, na baadhi wameamua kuchukua hatua mbalimbali kuonyesha hawana ubaya na Rais Uhuru Kenyatta.

Mbali na maseneta wawili kuandika barua kwa chama cha Jubilee kuomba msamaha kwa kukwepa mkutano ulioitishwa na Rais Uhuru Kenyatta wiki hii, viongozi wengine wameanza kuonyesha dalili za kujutia uamuzi wake.

Ijumaa, seneta maalum, Naomi Jillo Waqo, ambaye pia yupo kwenye orodha ya wale waliokosa kuhudhuria mkutano wa chama Ikuluni Jumanne, amesema uaminifu wake bado upo kwa Rais Kenyatta.

Seneta huyo na wenzake wanne waliandikiwa barua na chama ili waeleze kwa nini hawakufika kwenye mkutano, licha ya kupokea mwaliko. Aidha, wapo hatarini kufurushwa chamani na kupokonywa nyadhifa zao iwapo watapatikana na hatia.

Mnamo Jumatano, seneta Christine Zawadi alisamehewa baada ya kuandika barua ya kuomba radhi kwa Kiranja mpya wa Seneti, Irungu Kang’ata.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari jana, Bi Waqo alisema hakuweza kusafiri hadi Nairobi kuhudhuria mkutano huo kutokana na sababu ambazo wakuu wa chama wanazifahamu.

“Ningependa kusema kuwa mimi ni mtiifu kwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye ni kinara wa chama chetu. Niliwasilisha udhuru wangu na ukapokelewa Mei 11, 2020 na ninaunga mkono yaliyofikiwa mkutanoni,” akasema.

Wengine walio kwenye orodha ya maseneta waliotakiwa watoe sababu kwa nini wasitimuliwe ni; Millicent Omanga, Iman Falhada Dekow, Victor Prengei na Mary Yiane.

“Iwapo wanafikiria kwamba tutafanya makosa kama ODM na ANC na kuchukua muda mwingi kuwatimua, basi wanafaa wajua kwamba, tumejifunza na tunaenda kufuata mchakato unaohitajika ili adhabu itolewe haraka iwezekanavyo,” Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju aliambia Taifa Leo.

Onyo hili limewafanya wafuasi wengine wa Dkt Ruto kubadili picha zao kwenye mitandao na kuweka zile ambazo zinawaonyesha wakiwa karibu na Rais.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Aden Duale, Mbunge Maalum David Ole Sankok na Seneta Omanga ni miongoni mwa waliochukua hatua hiyo.

Bw Tuju alisema kwamba, ilikuwa vibaya kwa maseneta kususia mkutano wa Rais na lazima wajitayarishe kufika mbele ya kamati ya nidhamu chamani. Bw Tuju pia alisisitiza kwamba wamethibitisha kutoka kampuni za mawasiliano kwamba mialiko ilitumwa kwa maseneta wote wa Jubilee.

Hata hivyo, haijabainika iwapo Bi Waqo atasamehewa kwa kuwa alikuwa ameshapata barua kutoka kwa Kiranja wa wengi, Bw Kang’ata akitakiwa afike mbele ya kamati ya nidhamu.

“Chama kitatoa uamuzi kuhusu suala hilo baada ya kusikia kilio chake,” akasema Bw Kang’ata.

Bw Tuju naye alisema suala hilo limetoka mikononi mwake na sasa linashughulikiwa na kamati ya nidhamu chamani.

“Majina yaliwasilishwa mbele ya kamati ya nidhamu ya chama na njia ya kujinasua ni kuruhusu mchakato hitajika ukamilike,” akasema.

Bw Kang’ata alithibitisha kwamba amepokea msamaha wa Bi Jillo na kuuwasilisha kwa kamati ya nidhamu.

“Ni kamati ya nidhamu ambayo itatoa uamuzi. Mimi ni mlalamishi tu kwa niaba ya Seneti,” akasema.