• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Gor Mahia na Bandari FC kukosa fedha za CAF za mfuko wa kukabili Covid-19

Gor Mahia na Bandari FC kukosa fedha za CAF za mfuko wa kukabili Covid-19

Na GEOFFREY ANENE

WAWAKILISHI wa Kenya katika soka ya Bara Afrika ya msimu 2019-2020, Gor Mahia na Bandari wanasalia kumeza mate wengine wakila nyama baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutangaza mipango ya kuanza kupatia timu zilizofika 16-bora fedha kukabiliana na makali ya ugonjwa wa Covid-19.

Mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor, walibanduliwa nje ya Klabu Bingwa Afrika katika mechi za mwondoano walipocharazwa na USM Alger kutoka Algeria kwa jumla ya mabao 6-1.

Wangepiga USM Alger, wangetinga mechi za makundi na kujihakikishia Sh59 milioni.

Vijana hao wa kocha Steve Polack, ambao walikuwa wamenyuka Aigle Noir ya Burundi 5-1 katika mechi ya kuingia raundi ya kwanza kabla ya kusimamishwa na USM Alger 6-1, waliteremka katika Kombe la Mashirikisho (Confederation Cup).

Hata hivyo, walipoteza fursa nyingine ya kuingia mechi za makundi za mashindano hayo ya daraja ya pili walipokubali kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Kwa kufanya hivyo, walikosa tuzo ya Sh29.4 milioni.

Bandari, ambayo ilishinda Kombe la Rais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF Cup) na kuwakilisha Kenya katika Kombe la Mashirikisho, ilipita awamu mbili za kwanza za mashindano hayo vyema.

Iliondoa Wasudan Al-Ahly Shendi kupitia bao la ugenini baada ya kutoka 1-1 katika raundi ya kwanza.

Ilichapa Watunisia US Ben Guerdane kwa jumla ya mabao 3-2 katika raundi ya kwanza, lakini ikalemewa na Horoya kutoka Mali 5-2 katika mechi ya muondoano ya kuingia makundini.

“Soka kote duniani ikiwemo barani Afrika inapitia wakati mgumu. Hali ya sasa imekuwa na athari kubwa kwa wadau wetu. CAF inafahamu hali hii na itanusuru klabu, ambazo pia ni wadau wetu, kwa kupatia zilizofika mechi za makundi tuzo zao mapema,” Rais wa CAF, Ahmad Ahmad amenukuliwa na tovuti ya shirikisho hilo akisema Jumamosi.

Kwa kawaida, klabu hupata tuzo zao baada ya msimu wa mashindano kutamatika. Msimu 2019-2020 ulikatizwa kabla ya hatua ya nusu-fainali kutokana na virusi hatari vya corona. Msimu 2018-2019, Gor ilipata angaa Sh37 milioni kwa kufika robo-fainali ya Confederation Cup.

Ilikuwa imepokea Sh29 milioni katika mashindano hayo ya daraja ya pili mwaka 2018.

You can share this post!

Son Heung-min arejea Spurs baada ya kutumikia jeshi la...

Mikakati ipo kulainisha sekta ya utalii baada ya kunywea

adminleo