AKILIMALI: Mchungaji aingia karakana kuunda 'vigoda' vya mitungi ya maji kukalia
Na LAWRENCE ONGARO
HUKU hali ya maisha ikizidi kubana watu kutokana na athari za Covid-19, mchungaji mmoja wa kanisa ameamua kufanya kazi tofauti.
Mchungaji Raphael Ndung’u wa kanisa la Faith Impact Outreach Church eneo la Gatundu Kaskazini ameamua kuunda vifaa vya vyuma – ‘vigoda’ – vinavyotumika kuweka matangi ya maji safi yanayotumika kudumisha usafi kuzuia maambukizi ya Covid-19.
Anasema ujuzi wake wa kuchomelea vyuma haungepotea bure ndiposa ameamua wakati huu autumie kikamilifu.
Anasema yeye kama mchungaji amekosa kuhubiria waumini wake kwa miezi miwili sasa ingawa haelezi kwa nini hatumii vifaa na mitambo ya kiteknolojia kuifanya kazi hiyo.
“Baada ya serikali kupiga marufuku watu kujumuika pamoja kwa vikundi, mambo yetu kwetu baadhi ya wachungaji yamekwama,” anasema mchungaji Ndung’ u.
Sasa ameamua kuingia katika karakana ili afanye kazi ya ufundi kumwezesha kujikimu kimaisha.
Anawashauri wachungaji wenzake wabuni mbinu mpya za kujikimu kimaisha na waache dhana ya kutegemea waumini wao kuwatumia pesa kupitia simu. Kiufupi anawataka wasiwe tu wategemezi.
“Mungu amenijalia njia mpya ya kujikimu kimaisha na kwa hivyo sitaki kulaza damu bure,” akasema mchungaji huyo.
Anatoa mfano wa maandiko katika kitabu cha Mitume 18: 1-3 ambayo yanasema mwandishi Paulo aliunda hema ili kujiendeleza kimaisha na kunufaisha watu wengine.
Anatoa mwito kwa serikali iruhusu Wakristo warejee katika makanisa japo kwa masharti.
“Iwapo serikali itatukubalia kurejelea mahubiri yetu bila shaka tutafuata masharti yote yaliyowekwa ya kunawa mikono kila mara, kuvalia barakoa, na la muhimu zaidi kuweka nafasi ya mita moja au zaidi kutoka mtu mmoja hadi kwa mwingine,” akafafanua.
Hapo matamshi yake yakaungwa mkono na mshiriki wake wa kanisa ambaye alisema tangu waumini waache kuhudhuria ibada wengi wao ‘wamemsahau’ Mungu wakichukulia maombi kwa mzaha.
Mchungaji Ndung’u anasema vifaa alivyounda vitakuwa na umuhimu wake hata wakati corona itapungua na mambo kurejea ya kawaida.
Anavisifu kwamba vimeundwa kwa ustadi mkubwa ambapo kabla ya mtu kunawa anabonyeza eneo fulani akitumia guu lake huku sabuni ikitokea upande mwingine ambapo inakuwa kwamba maji yanatiririka bila kushika na mkono.
Anawahimiza watu wote waliopoteza ajira zao kutokana na athari za corona wawe wabunifu na kuona ya kwamba wanatafuta jambo la kufanya badala ya kulaumu serikali kwa sababu janga hilo “limetuvamia ghafla bila ya sisi kutarajia.”
“Tunajua ni kugumu kimaisha lakini serikali haiwezi ikafanikiwa kuufikisha mkono wake wa msaada kwa kila mmoja kila wakati na kwa hivyo tujitafutie mbinu za kuishi kwa wakati huu,” akashauri.