Michezo

PWEZA AJIPALIA MAKAA: Tashtiti ya Lacazette kuvuta gesi ya kumfanya mtu acheke 'Nitrous Oxide'

May 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHRIS ADUNGO na MASHIRIKA

ARSENAL wameapa kumwadhibu vikali mshambuliaji wao matata Alexandre Lacazette baada ya kuibuka kwa ripoti kwamba nyota huyo mzawa wa Ufaransa alipatikana akivuta gesi ya Nitrous Oxide almaarufu ‘Laughing Gas’ iliyokuwa imejazwa ndani ya puto.

Gazeti la Daily Star nchini Uingereza lilichapishwa makala zenye picha zilizoonyesha Lacazette akiwa na puto yenye gesi hiyo mdomoni. Baadaye, sogora huyo wa zamani wa Olympique Lyon, Ufaransa aliwatumia wanasoka wenzake wa Arsenal video iliyochukuliwa akivuta gesi hiyo kupitia mitandao ya kijamii.

Ingawa msemaji wa Arsenal, ameshikilia kwamba tukio hilo ni “suala la kibinafsi” litakaloshughulikiwa na klabu katika kiwango cha “ndani kwa ndani”, huenda Lacazette “akapigwa bakora”.

Ni wiki moja pekee imepita tangu Lacazette apatikane miongoni mwa wanasoka wengine wa Arsenal waliokiuka kanuni mpya za afya zinazodhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya corona.

Lacazette, 28, alionekana akiwa karibu sana na mwanamume mmoja aliyekuwa akimwoshea gari lake jijini Londo, Uingereza. Hivyo, alivunja kanuni inayotaka mtu kudumisha umbali wa hadi mita mbili kati yake na mwingine.

Mbali na Lacazette anayehusishwa na uwezekano mkubwa wa kuyoyomea Uhispania kuchezea Barcelona mwishoni mwa msimu huu, wengine waliokiuka kanuni hiyo ni David Luiz, Nicolas Pepe na Granit Xhaka.

Kwenye picha zilizosambaa mitandaoni, Luiz na Xhaka walionekana wakikaribiana sana walipokuwa wakiponda raha katika bustani moja jijini London huku Pepe akionekana akicheza mpira pamoja na marafiki zake.

Wanne hao walionywa huku usimamizi wa Arsenal ukiapa kutoa adhabu kali zaidi kwa yeyote atakayekiuka kanuni ambazo zimewekwa na serikali ya Uingereza katika juhudi za kukabiliana na corona.

Wiki moja imepita tangu Arsenal warejee kambini kuanza mazoezi katika uwanja wa London Colney, Uingereza kwa minajili ya mechi zilizosalia katika kipute cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu

Idadi ya wachezaji ambao wamekuwa wakitumia uwanja huo kwa wakati mmoja imedhibitiwa huku mazoezi yakiendeshwa kwa utaratibu wa watu kudumisha umbali wa mita moja kati yao.

Isitoshe, majengo yote yaliyoko katika eneo la Colney yamefungwa na wachezaji wamekuwa wakisafiri mmoja mmoja katika magari yao binafsi na kurejea nyumbani moja kwa moja baada ya kukamilisha vipindi vya mazoezi.