• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Obiri kustaafu riadha akivunja rekodi ya dunia katika mbio za mita 5,000

Obiri kustaafu riadha akivunja rekodi ya dunia katika mbio za mita 5,000

Na CHRIS ADUNGO

HELLEN Obiri na Faith Kipyegon ni miongoni mwa Wakenya waliokuwa wafungue kampeni za Diamond League mjini Shanghai, China wikendi iliyopita kabla ya kivumbi hicho kuahirishwa hadi Septemba 19, 2020.

Kipyegon ambaye ni bingwa wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500 ana matarajio ya kurejea Shanghai kwa matao zaidi hasa ikizingatiwa kwamba ndiko alikowahi kuandikisha muda bora zaidi wa kibinafsi katika mbio hizo za mizunguko minne mnamo 2016.

Ushindi wa Kipyegon katika kivumbi hicho kunatarajiwa kumtia hamasa ya kutamba hata zaidi kwenye Olimpiki zitakazoandaliwa Tokyo, Japan mnamo 2021.

“Nilikuwa na mbio hizi za Shanghai akilini mwangu nilipokuwa mazoezini. Nilitaka sana kutawala kivumbi hiki cha Diamond League nchini China. Hata hivyo, janga la corona limeahirisha mambo,” akasema Kipyegon.

Zaidi ya Shanghai kumpa majukwaa ya kuweka rekodi za muda wake bora zaidi katika nyakati mbalimbali, Kipyegon aliwahi kuandikisha rekodi ya dakika 3:56.82 katika historia yam bio hizo mnamo 2016.

“Huo ni muda wa kasi sana, lakini niliuboresha zaidi hadi dakika 3:54.22 niliporejea kutoka likizo ya uzazi na kujinyakulia nishani ya fedha katika Riadha za Dunia za 2019 jijini Doha, Qatar,” akasema Kipyegon alipokuwa akihojiwa na gazeti moja la Kenya.

Kwa upande wake, Obiri amekuwa akishiriki mazoezi makali kwa nia ya kuweka muda bora zaidi katika mbio za mita 5,000. Mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 30 amesema kwamba angali na matarajio makubwa ya kujinyakulia dhahabu katika Olimpiki zijazo za Tokyo.

Hata hivyo, Obiri anashikilia kwamba mabadiliko kwenye kalenda iliyotolewa majuzi na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) yatawapa wanariadha wengi ugumu wa kurejea katika hali zao bora zaidi kabla ya kivumbi cha kwanza cha Diamond League kuandaliwa jijini Olso, Norway mnamo Juni 11, 2020.

Kubwa zaidi katika maazimio ya Obiri ni kuvunja rekodi ya dunia ya muda wa dakika 14:11.15 katika mbio za mita 5,000 kabla ya kustaafu rasmi ulingoni. Rekodi hiyo imekuwa ikishikiliwa na Mwethiopia Tirunesh Dibaba tangu mwaka wa 2008.

Muda wa kasi zaidi katika historia ya mbio hizo unajivuniwa na Waethiopia wakiwemo Almaz Ayana (14:12.59) na Meseret Defer (14:12.88).

Muda wa dakika 14:18.37 ulioandikishwa na Obiri jijini Roma, Italia mnamo 2017 ndio wa tano kwenye orodha ya muda bora zaidi katika historia ya mbio hizo.

Mwaka 2019 jijini London, Uingereza, Obiri alichomoka mbele ya Mholanzi Sifan Hassan katika mbio za mita 5,000 na kuandikisha muda wa dakika 14:20.36. Hiyo ilikuwa rekodi mpya katika historia ya duru za Diamond League jijini London na wa kasi zaidi katika mwaka wa 2019.

Mkenya mwingine, Agnes Tirop aliyeibuka wa pili katika mbio hizo, alisajili muda wa dakika 14:20.68 ambao ulikuwa wa pili kwa kasi zaidi mnamo 2019.

“Tutajitahidi kuzoea mabadiliko ya msimu mpya. Bila shaka natazamia kuboresha muda wangu binafsi na kuvunja rekodi ya dunia ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka 10. Nikifaulu kwa hilo, nitastaafu sasa kwa amani,” akasema Obiri ambaye kwa sasa anapania kuboresha kasi yake zaidi kwa kushiriki mazoezi ya hadi kufikia mita 3,000 kwa siku.

You can share this post!

UBOMOAJI: Matiang’i na wenzake wakaidi seneti

Polisi wampiga risasi babake seneta wa Lamu kwa kutovaa...

adminleo