Habari

IEBC yaanika uozo wake

May 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DAVID MWERE

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imejipata pabaya baada ya kuanika uozo kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2017.

Ni kutokana na ufichuzi huo ambapo wanasiasa sasa wanataka tume hiyo ifanyiwe mageuzi makubwa kabla ya uchaguzi Mkuu wa 2022.

Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna na Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior ni baadhi ya viongozi ambao wanashinikiza kutekelezwa kwa mageuzi hayo.

Data hiyo ilikuwa imechapishwa katika mtandao wa IEBC miaka mitatu iliyopita na iliondolewa juzi baada watu kugundua kwamba ilikuwa imejaa kasoro tele.

Seneta Kilonzo na Bw Sifuna walikasirishwa na IEBC na kushangaa kwa nini imechukua miaka mitatu kuiondoa, ilhali ilikuwa na makosa hasa kuhusiana na walioshinda nyadhifa mbalimbali za kisiasa.

Dosari hilo pia imetia doa utendakazi wa IEBC inayoongozwa na Wafula Chebukati.

Bw Kilonzo Jnr jana alifafanua kwamba kasoro hiyo imesababishwa na hatua ya IEBC kukataa kutumia mbinu ya teknolojia ya EMS, hasa wakati wa kutoa matokeo.

“Linalojitokeza sasa inasikitisha na linaonyesha wazi ukora uliokuwa umekithiri IEBC. Mageuzi makubwa tunayahitaji kwa sasa katika tume hiyo,” akasema Bw Kilonzo Jnr.

Kando na Bw Chebukati, makamishina wengine wanaohudumu kwa sasa ni Boya Molu na Abdi Guliye, baada ya wengine kujiuzulu miaka miwili iliyopita.

Kulingana na sheria za uchaguzi za 2017, EMS ilifaa kukagua data hiyo baada ya mwaka moja, muda huo ukiwa ni 2018.

Kikatiba IEBC ina jukumu la kuandaa uchaguzi, kura ya maamuzi na kuweka mipaka mipya katika maeneo ya uwakilishi.

“IEBC kwa sasa inafaa kufanyiwa mageuzi baada ya baadhi ya makamishna wake na naibu mwenyekiti kuondoka. Pia makosa asasi zake za kutatua mizozo inayotokea wakati wa uchaguzi,” akasema Bi Waiguru.

Kwenye data iliyoondolewa, Mbita bado inarejelewa kama eneobunge ilhali IEBC yenyewe ilibadilisha jina lake na kuchapisha Suba Kaskazini kama jina lake jipya.

Ingawa Millie Odhiambo alitangaza mshindi wa kiti hicho cha ubunge kupitia chama cha ODM, data iliyoondolewa ilisema aliwania kwa tiketi ya ANC na kupata kura 65 pekee. Data hiyo inaonyesha mbunge wa eneo hilo ni Noah Odhiambo ambaye alipata kura 27,208 kupitia ODM.

Kwenye kasoro nyingine, Eve Obara ndiye Mbunge wa Kasipul Kabondo kupitia ODM ilhali data is IEBC ilikuwa ikionyesha Silvance Osele kama mshindi kupitia ODM kwa kura 27,496.

Data hiyo inaonyesha Bi Obara aliwania kupitia chama cha Jubilee na kupata kura 69 ilhali hakuna uchaguzi mdogo uliowahi kuandaliwa Kasipul Kabondo.