TAHARIRI: Maski: IPOA ikabili polisi wasumbufu
Na MHARIRI
KWA karibu miezi mwili sasa, serikali imeendeleza masharti ya kuhakikisha wananchi wanajilinda na kuwalinda wenzao dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Mbali na kutangaza kafyu na kuwataka watu wanawe mikono, serikali ilitangaza kwenye kanuni za wizara ya Afya kwamba ni lazima kila mtu avae barakoa au maski katika maeneo ya umma.
Sababu ya watu kulazimishwa kuvaa barakoa ni kuhakikisha wanapokohoa, kuzungumza au kuchemua, majimaji yanayosemekana kuwa na virusi hivyo hayatawafikia wengine na kuwaambukiza.
Wakati mwingine, kutokana na sababu mbalimbali, mtu anaweza kukosa kuvaa barakoa. Kwanza kuna suala la kupatikana kwa barakoa hizo. Waziri wa Ustawi wa Viwanda, Bi Betty Maina aliahidi kuwa barakoa zingepatikana kwa Sh20. Ahadi hiyo haijatekelezwa kufikia leo, na barakoa rahisi zaidi ni ya Sh50.
Wakati huu ambapo Wakenya wengi hawaendi kazini na biashara haziendi vizuri, kuna uhaba mkubwa wa pesa. Kumtarajia mtu kutenga bajeti ya Sh50 kila siku kwa niaba yake na familia yake badala ya kununua chakula, ni kuwa na matarajio ya kupita kiasi.
Lakini hata wakio na uwezo wa kuzinunua barakoa, yawezekana wasizivae kwa sababu nyingine. Kwa mfano mjini Nyeri, polisi walimkamata mkazi kwa kutovaa barakoa alipokuwa anakula chakula ndani ya mkahawa.
Ni wazi kuwa mtu anapokula hutumia mdomo. Barakoa huziba pua na mdomo. Mtu atakula vipi? Isitoshe, kwenye mikahawa wateja wanatenganishwa umbali ambao hata mmoja akichemua kwa bahati mbaya, hataweza kuambukiza wateja wengine.
Inaudhi kwamba maafisa wa polisi wameamua kutumia sheria hii ya watu kuvaa barakoa kama kitega uchumi. Badala ya kuwashika wahusika na kuwapeleka wanakostahili, maafisa wengi sasa huitisha hongo.
Baya zaidi ni utumizi wa silaha dhidi ya watu kama hao. Haieleweki ni kwa nini polisi walilazimika kutumia risasi, lakini hata kama walikuwa na sababu za kueleweka, huo ni utumizi mbaya wa silaha. Kanuni zilizopo hazijaidhinisha polisi kujeruhi raia.
Tume ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA), yafaa kuchunguza kisa cha kupigwa risasi babake Seneta wa Lamu, Bw Anwar Loitiptip. Maafisa watakaopatikana na hatia ya kuhusika katika kitendo hicho, wachukuliwe hatua kulingana na sheria.