• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Mama mboga watwangana sokoni

Mama mboga watwangana sokoni

Na TOBBIE WEKESA

GIKOMBA, Nairobi

KIOJA kilizuka sokoni baada ya akina mama mboga wawili kupimana nguvu hadharani waking’ang’ania wateja.

Inasemekana mama hao ambao wameuza katika soko hilo kwa muda walirushiana makonde bila kuwaogopa wateja wao.

Kwa mujibu wa mdokezi wetu, mzozo ulianza baada ya mama mmoja kuibua madai kwamba mwenzake anatumia juju kuvutia wateja kwenye kibanda chake.

Hii ni baada yake kuona kwamba wateja walikuwa wakibanana katika kibanda cha mwenzake, ilhali kwake hapakuwa na yeyote.

“Kwani huyu mama anauza nini ambacho sisi wengine hatuna. Mbona wateja wengine wasije hapa kwangu niwauzie,” akawa akiuliza mara kwa mara.

Siku ya tukio alishindwa kuvumilia akaelekea kwa mwenzake na kuanza kumrushia maneno.

“Kwani hili soko lote ni wewe tu unauza bidhaa. Tuko na vitu vinavyofanana mbona wateja wapige foleni kwako ilhali sisi wengine hatuna wateja. Wewe unatumia juju,” alifoka.

Mwenzake akainuka.

“Unaambia nani hivyo. Wewe mwenyewe umetembea kwa waganga mpaka nguo zimekuisha mwilini. Peleka ujinga mbali!”

Mama mbishi alimrukia na kuanza kumzaba makofi; wa pili akajibu mapigo na kukazuka vita vikali huku wateja wakiwatazama kwa mshangao na baadhi wakicheka.

“Kila siku ninakuja sokoni lakini vitu vyangu havinunuliwi ilhali vyako vinaisha. Hiyo juju yako lazima utaitoa ama uhame soko hili,” mama mlalamishi akadai.

Wawili hao waliendelea kuchapana makonde huku wakiraruliana mavazi.

“Hapa sihami. Mbona usijiulize kwanini wateja hawakupendi. Shetani aliyekutuma kwangu hana bahati,” mwenzake akamjibu.

Wateja waliamua kuingilia kati baada ya kuona wakiumizana na kuaibishana.

“Huyu mwanamke ni mshenzi sana. Ana wivu na tabia mbaya ndio maana wateja hawampendi. Kwenda kabisa,” mama wa pili alilipuka.

Lakini wa kwanza aliapa kumtimua iwapo hali itaendelea kuwa vile. “Wewe na juju zako lazima mtaenda upende usipende!”

You can share this post!

UDAKU: Ni rasmi Usain Bolt ni baba

ONYANGO: Ruto hana jingine ila kuunda chama kipya

adminleo