Makala

NASAHA ZA RAMADHAN: Tumeingia katika kipindi cha lala salama, tusilegeze kamba

May 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SHEIKH MOHAMED KHALIFA

KWA mapenzi ya Mwenyezi Mungu tumebakisha siku zisizozidi tano.

Huu ni ule muda ambao kama ni kwenye mchezo wa kandanda, ni kipindi cha lala salama.

Maswali tuliyopokea leo kwa jumla yanahusiana na jinsi ya kujiandaa na sikukuu ya Eid-Ul-Fitri.

Maswali haya, nitayajibu kwa awamu mbili Insha-Allah.

Katika awamu ya kwanza, nitachukua fursa hii nitoe nasaha kwa wasomaji na Waislamu kwa jumla kuhusiana na masuala haya.

Nimetangulia kusema kwamba tupo kwenye kipindi cha lala salama. Kama ni katika mbio, mkimbiaji anapoukaribia utepe huongeza bidii zaidi. Kama ni mbio fupi kama mita 100 ambapo karibu kila mkimbiaji hukaribia kamba au mstari kwa kukaribiana, mtu anaweza kutumia hata kifua, kichwa au mguu kuibuka mshindi.

Hivi ndivyo ilivyo Ramadhani na ibada ya saum. Wapo watu ambao mwezi ulipoandika mwishoni mwa Aprili, walijitokeza kwa wingi na kufunga kwa dhati. Ingawa hakuna watu kuswali misikitini, kuna watu wengi ninaowajua ambao walijikita kwenye ibada ya kuswali ndani ya nyumba zao na familia zao.

Hali hiyo huenda si hivyo tena. Kutokana na maswali tunayopokea, ni dhahiri kuwa baadhi ya Waislamu wameondoa fikira zao katika kung’ang’ana ili kuwa wa kwenye utepe. Wameanza kufikiria ni jinsi gani watawanunulia watoto wao nguo za sikukuu ilhali baadhi ya maeneo ambayo kawaida huwa na bei rahisi yamefungwa.

Tayari akina mama wengi kwenye miji kama Mombasa, wanatumia muda wao mwingi wakizunguka kwenye maduka kutafuta nguo kwa watoto wao badala ya kutumia siku hizi zilizosalia kutia bidii katika ibada.

Mtume Muhammad (SAW) katika siku kama hizi, alikuwa akijikaza zaidi na kutenga muda mwingi kukamilisha ibada. Huu ndio wakati wa kupambana na nafsi zetu na kuzidisha kuomba msamaha.

Itakuwa hasara kubwa ikiwa kwa mfano usiku wa Laylatul Qadr utakuwa haujapita, na kwa kulegea kwetu, uje na kuondoka bila ya sisi kunufaika nao.