• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:10 PM
COVID-19: Waandishi wanaofanyia kazi eneo la Thika wataja masaibu yao

COVID-19: Waandishi wanaofanyia kazi eneo la Thika wataja masaibu yao

Na LAWRENCE ONGARO

BARAZA la Vyombo vya Habari Nchini (MCK) linazidi kufuatilia jinsi waandishi wa habari mashinani wanavyoendesha kazi zao.

Mnamo Jumanne afisa wa kitengo cha fedha katika MCK Bw George Maina alizuru Thika, Kaunti ya Kiambu na kufanya kikao cha dharura na waandishi wapatao 15 kwa lengo la kufahamu changamoto zao hasa wakati huu mgumu wa kupambana na Covid-19.

Huku waandishi hao wakifuata maagizo yote ya kiafya ya kuvalia barakoa, kunawa mikono na kukaa umbali wa mita moja au zaidi kati ya mmoja hadi kwa mwingine, walikuwa na mengi ya kunena.

Cha muhimu katika kikao hicho ni kuwa wengi wao kukosa vitambulisho maalum wakati huu wa kukabili Covid-19 vinavyotumika kwa sasa kote nchini na waandishi wa habari.

Jambo lingine lililoangaziwa ni fedha za usafiri na kujikimu wakati wa kwenda kutafuta habari hizo sehemu za mbali.

Ilithibitishwa ya kwamba katika vizuizi hivyo vya polisi waandishi wengi wa mashinani wanakwaruzana na maafisa wa usalama kwa sababu ya kanuni na sheria mpya zilizowekwa hivi majuzi.

Walisema inakuwa vigumu kupita katika vizuizi hivyo vilivyowekwa maeneo tofauti.

Walilalama kabla ya kuelewana na maafisa hao, huwa inachukua muda mrefu.

Waandishi wanastahili kupata vifaa vyote vya kujikinga kuepukana na Covid-19.

Kwa muda wa miezi miwili iliyopita waandishi wengi wamepitia masaibu mengi ya kifedha kwani pia wana familia zinazowategemea na kipato wanachopata ni kidogo mno.

Walisema mara nyingi waandishi wa mashinani hulazimika kupiga masafa marefu ili kutafuta habari lakini wakati mwingine hata wanakosa nauli kufika sehemu zingine.

Kwa hivyo, kwa maoni yao waliwasilisha matakwa hayo kwa MCK ili ifanye jambo kwa haraka ili waweze angalau kujikimu kimaisha.

Hata hivyo Bw Maina aliyefika kusikia malalamishi hayo alisema tayari shirika hilo la MCK linazunguka nchini kote ili kupata picha safi kuhusu hali ya waandishi wa mashinani.

“Tunaelewa kuna shida kubwa hata waandishi walio kwenye ofisi tunajua sasa wanapitia hali ngumu lakini MCK inatafuta mbinu jinsi itakavyokabiliana na hali hiyo,” akasema Bw Maina.

Alisema wanajaribu kuwasiliana na mashirika mengine ya nje ili kutafuta mbinu ya kupata fedha za kuwasaidia waandishi.

Alisema siku chache zilizopita wamewasaidia waandishi kadha na fedha chache za kujikimu.

Bw Maina aliwahakikishia waandishi hao ya kwamba kwa muda chini ya wiki moja watafanya juhudi kuona ya kwamba waandishi wa Thika wanapata vitambulisho maalum vya kuangazia Covid-19 ili kurahisisha kazi yao katika mashinani.

Baada ya kusikiza matakwa ya waandishi wa Thika, afisa huyo alifululiza hadi Murang’a ili kupata maoni ya waandishi wa huko.

You can share this post!

Kesi ya rufaa ya Manchester City dhidi ya marufuku ya Uefa...

Presha zaidi kwa Ruto

adminleo