• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
COVID-19: Kampuni za kamari zatoa mchango wa Sh5m ziwafae wanamichezo

COVID-19: Kampuni za kamari zatoa mchango wa Sh5m ziwafae wanamichezo

Na GEOFFREY ANENE

CHAMA cha kampuni za kamari nchini Kenya kimeongeza Sh5 milioni katika mfuko wa serikali wa kusaidia wanamichezo kukabiliana na makali ya janga la virusi hatari vya corona.

Virusi hivyo, ambavyo vinahangaisha dunia nzima, vimeua watu 50 nchini Kenya, huku visa vya maambukizi vikifika 912 Jumatatu.

Wizara ya Michezo, Utamaduni na Sanaa imesema kuwa Sh5 milioni ilizopokea Mei 18 ni kando na Sh15 milioni ambazo kampuni ya kubahatisha matokeo ya mechi ya Betika ilitoa wiki chache zilizopita.

“Tunashukuru washirika wetu kutoka michezo kwa michango yao wakati huu muhimu kwa juhudi za kampuni zilizojitolea kibinafsi,” taarifa kutoka wizara hiyo imesema.

“Wizara itapeleka fedha hizi kwa wanamichezo wenye shida siku chache zijazo mara tu tutakapokamilisha shughuli ya kuwatambua na kuwakagua kwa kushirikiana na mashirikisho husika. Tunapatia kipaaumbele wanamichezo ambao hawana njia nyingine ya kujitafutia riziki, wale ambao wako katika timu zetu za taifa na wale ambao bado wanajishughulisha na uchezaji ambao wako katika timu ya Kenya,” waziri Amina Mohamed alisema kabla ya kuongeza kuwa kuna mipango ya kusaidia wanamichezo walio nje ya kundi hilo mara tu mfuko wa fedha hizo utakuwa mzuri zaidi.

“Tungependa mashirikisho ya michezo yatupatie takwimu sawa haraka iwezekanavyo ili tuhakikishe kuwa watu wanaolengwa wanapata misaada hii,” alisema. Wizara hiyo pia imeomba wahisani waendelee kusaidia wanamichezo kote nchini kwa kuwapa vyakula, kusambaza vyakula katika sehemu zinazohitaji na pia kifedha.

You can share this post!

Ofisi ya msajili yasimamisha ndoa tena

Zarika asema ana kiu ya kuvaana na bingwa WBC Yamileth...

adminleo