Ujerumani yaifaa Kenya vituo viwili vya maabara tamba kupima Covid-19
Na SAMMY WAWERU
KENYA imepokea msaada wa vituo viwili vya maabara tamba kupima Covid-19 kutoka kwa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani ili kusaidia mikakati ya kudhibiti msambao wa ugonjwa huu nchini.
Akizungumza Jumatano wakati wa kupokea vituo hivyo pamoja na vifaa vingine kupima virusi vya corona katika makao makuu ya Wizara ya Afya, Nairobi, Waziri Mutahi Kagwe amesema kituo kimoja kitapelekwa eneo la mpaka wa Namanga unaounganisha Kenya na Tanzania na kingine mjini Naivasha.
“Vitatusaidia kupima madereva katika kituo cha mpaka eneo la Namanga na mjini Naivasha,” waziri akasema, akimiminia sifa serikali ya Ujerumani, kwa ushirikiano wake na Kenya katika kuimarisha mikakati kudhibiti maambukizi wa Covid – 19 nchini pamoja kusaidia kustawisha uchumi.
Msaada huo umetolewa kupitia afisi ya Ubalozi wa Ujerumani nchini Kenya.
“Vituo tamba hivi pamoja na vifaa vingine vitasaidia kurahisisha shughuli za upimaji wa virusi hivi na magonjwa mengine enezi,” amesema Balozi wa Ujerumani nchini Kenya Annett Günther.
Jumuiya ya Afrika Mashariki pia imepokea vituo tamba tisa, Waziri wa EAC Adan Mohamed akisema changamoto zinazoshuhudiwa maeneo ya mipakani zitatatuliwa.
Msaada huo umekuja siku kadhaa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kufunga mipaka inayounganisha Kenya na Tanzania na vilevile ya Somalia, kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi ya Covid-19 miongoni mwa madereva.
Rais alisema malori ya kusafirisha mizigo ndiyo pekee yataruhusiwa kuingia nchini.
Ni hatua iliyozua tumbojoto kati ya Kenya na Tanzania, taifa hilo jirani likipiga marufuku madereva wa Kenya kuingia humo.
Leo Jumatano Kenya imethibitisha visa vipya 66 vya Covid-19 idadi jumla tangu Machi 13, 2020, ikifika 1,029.