• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
COVID-19: Mwanadada atia fora Mombasa katika maandishi na uchoraji kuhamasisha jamii

COVID-19: Mwanadada atia fora Mombasa katika maandishi na uchoraji kuhamasisha jamii

Na FARHIYA HUSSEIN

KAUNTI ya Mombasa imeanzisha mbinu ya kutumia sanaa za maonyesho kutoa hamasisho jinsi ambavyo wenyeji na wakazi wengine wanaweza kukabili ugonjwa wa Covid-19.

Mbinu hiyo inahusisha michoro na maandishi katika kuta za majumba yaliyoko upande upande wa barabara kadhaa kuonyesha watu jinsi wanavyostahili kujitunza kuepuka ugonjwa huo.

Ukitembea katika mitaa kadhaa Mombasa, unapatana na kazi mbalimbali za sanaa za maonyesho, hasa michoro na maandishi katika kuta, zikitoa ujumbe kuhusu janga la Covid-19.

Taifa Leo imepata fursa ya kumhoji Bi Ferdaus Ahmed, 19, mmoja wa vijana ambao wanaendeleza mradi huo wa michoro huku akiwa kijana wa pekee wa kike.

Mwanadada huyo anasema kusudi lake kuu la kujiunga na kikundi hicho lilikuwa kutaka jamii yake ipate mtazamo tofauti wa jinsi picha halisi ya mwanamke.

“Niligundua kuwa nina kipaji cha uchoraji nilipokuwa na umri wa miaka 14 na nikaamua kukikuza kwa kusomea zaidi sanaa hiyo,” akasema.

Akianza anasema alikabiliwa na changamoto kadhaa kabla ya kuamua kufanya sanaa hiyo kama kazi yake.

“Nilikuwa najifunza kutoka kwa video katika mtandao wa YouTube kabla ya kuenda shuleni kujifunza ili kubobea katika uchoraji,” akasema mwanadada huyu.

Anaeleza kuwa kazi yake ya kwanza ilikuwa mchoro wa kawaida unaojulikana kama turubai.

Ferdaus Ahmed,19, achora na kuandika katika ukuta mmojawapo wa jengo katika Kaunti ya Mombasa kueneza ujumbe wa hamasisho kukabili Covid-19. Picha/ Farhiya Hussein

Anaeleza jinsi alivyoungana na wenzake Mombasa.

“Niliziona picha zilizochorwa katika kuta tofauti za kaunti na kuvutiwa nazo. Hapo ndipo nikaamua kujiunga na wanaoendeleza shughuli hiyo ili kuwakilisha jinsia ya kike katika vita dhidi ya Covid-19,” akasema.

Ferdaus amechora na kuambatanisha maneno yeye peke yake katika ukuta mmoja ulioko karibu na eneo la Shariff Nasir kando ya Hospitali Kuu ya Pwani ujumbe ukiwa: ‘You cannot quarantine love’ yaani ‘Huwezi ukaweka upendo au mapenzi katika karantini’.

Kundi hilo lina vijana sita ambao wamejigawa katika makundi matatu.

Kikundi kimoja kinachora picha za sanaa eneo la Pandya na kingine karibu na Buxton eneobunge la Mvita.

Ujumbe wao unajumuisha maana tofauti.

“Sehemu moja inaonyesha utunzaji wa jamii, ambapo zingatio lipo katika haja ya umoja na kumjali mwenzako. Nayo nyigine inaonyesha jinsi wadau mbalimbali wanavyoshirikiana kupiga vita janga hili la Covid-19 ambapo tunaona mchoro wa gavana, afisa wa polisi, viongozi wa dini na raia,” akasema.

Ferdaus Ahmed,19, achora katika ukuta mmojawapo wa jengo katika Kaunti ya Mombasa kueneza ujumbe wa hamasisho kukabili Covid-19. Picha/ Farhiya Hussein

Kwa sasa, Ferdaus ni mwanafunzi katika taasisi ya Lotus iliyoko Dubai ambako anasomea Taaluma ya Sanaa lakini anasema safari yake ilikuwa yenye visiki tele; hasa vya watu wa kumhukumu vibaya na hata kukata tamaa kwake.

“Wengi wetu tuna talanta lakini baadhi ya wazazi hawatupi motisha. Ninamshukuru sana mama yangu hasa kutoka kwa jamii ambayo inaamini kuwa wanawake wanafaa kupika na si kufanya kazi za sanaa,” akasema.

Kulingana na Afisa Mkuu wa Utalii Kaunti hiyo, Bi Asha Abdi, Mradi wa Sanaa ya Mitaani ni kati ya majukwaa mengi yanayotumika kupitisha ujumbe wa Covid-19.

“Tumekuwa tukifanya tangazo kupitia vyombo vya habari na mahojiano ya redio kuelimisha wakazi juu ya umuhimu wa kufuata hatua zote zilizowekwa kupunguza kuenea kwa ugonjwa huo. Lakini vijana walipokuja na wazo hili la sanaa tuliwapa jukwaa la kuonyesha talanta zao pia,” akasema Bi Abdi.

Bi Abdi anasema walichagua eneo la Buxton kwani ni barabara iliyojaa waendeshaji magari na wakazi ambao wanatembea kwa miguu.

“Uchoraji umepokelewa vizuri. Tumeona watu wakipiga picha na mara nyingine wanasimama na kutazama ujumbe katika michoro hiyo. Upo mchoro wenye ujumbe unaoonyesha ushirikiano baina ya serikali ya kaunti na sekta mbalimbali ikiwemo ile ya binafsi, ya umma na Shirika la Msalaba Mwekundu,” akasema Bi Abdi.

Anasema sanaa ya aina hiyo pia huchangia pakubwa katika sekta ya utalii.

You can share this post!

COVID-19: Visa jumla nchini Kenya sasa ni 1,029

Himizo Waislamu watii masharti hata wakati wa sherehe za...

adminleo