Habari

Rajoelina asema amezungumza na WHO kuhusu 'dawa' ya Covid Organics

May 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

RAIS wa Madagascar Andry Rajoelina amesema Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeidhinisha mfumo wa siri (formula) wa utayarishaji wa dawa ya kienyeji ambayo taifa lake linadai ni tiba ya Covid-19.

Rais huyo alisema kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter kwamba alizungumza Jumatano kwa njia ya video na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus akisema shirika hilo pia limekubali kuunga mkono majaribio ya dawa hiyo barani Afrika.

Naye katika ujumbe katika akaunti yake ya Twitter, Tedros amethibitisha Alhamisi kuwasiliana na Rajoelina kuhusu hali ya Covid-19 nchini Madagascar.

“Tulijadili namna ya kushirikiana katika utafiti wa dawa na kwamba umoja ni hitaji muhimu katika vita dhidi ya janga hili na kuhakikisha kuwa ulimwengu ni salama,” akasema Dkt Tedros.

Hata hivyo, mkuu huyo wa WHO hakurejelea moja kwa moja dawa ya Madagascar kwa jina Covid Organics (CVO).

Haya yanajiri baada ya Rajoelina kutoa wito kwa wananchi wa Madagascar kunywa hiyo ‘dawa’ ambayo anadai ina uwezo wa kuzuia au kutibu ugonjwa huo.

“Nahimiza kwamba tunywe dawa hii ili tujikinge, tukinge familia zetu na majirani zetu…. na vifo havitashuhudiwa nchini,” Rais Rajeoelina akasema kwenye hotuba aliyotoa Jumapili, ilivyoripotiwa katika gazeti la kila siku la L’express de Madagascar.

Nchi hiyo iliyoko Kusini Mashariki mwa Afrika imenakili visa 304 vya Covid-19, kisa kimoja cha mtu kufariki na wagonjwa 114 kupona. Hii ni kulingana na data iliyokusanywa na Chuo Kikuu cha John Hopkins kilichoko Amerika.

Na mtu huyo mmoja aliyefariki amekuwa akiugua kisukari.

Rais Rajoelina alisema dawa ambayo inafanana na chai ya mkanda, inasambazwa kwa wananchi katika maeneo yaliyoshuhudia visa vingi vya maambukizi.

Kiongozi huyo alisema serikali yake inashirikiana na madaktari wa kigeni na wanasayansi wa kimataifa katika kuendeleza utafiti zaidi kuhusu ‘tiba’ hiyo.