COVID-19: Kenya ina jumla ya visa 1,109
Na MAGDALENE WANJA
WAKENYA wametakiwa waendendelee kuzingatia sheria zilizowekwa ili kuzuia maambukizi ya Covid-19.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema Alhamisi kuwa watu walioripotiwa kupona wanapaswa kujua kuwa wanaweza kupata maambukizi tena endapo hawatachukua tahadhari.
Waziri Kagwe amesema hayo wakati akithibitisha visa 80 vipya vya maambukizi ya ugonjwa huo. Hii inafikisha idadi ya walioambukizwa kufikia 1,109 nchini Kenya.
Visa hivi vipya ni pamoja na 41 kutoka Nairobi, 20 kutoka Mombasa na saba kutoka Kaunti ya Siaya.
Visa 13 vya maambukizi vimeripotiwa kutoka mtaa wa Kibra, Nairobi.
Kwale ina visa sita.
“Miongoni mwa waliopatikana na maradhi hayo ni wale waliosafiri kutoka mtaa wa Kibra, Nairobi kuelekea Siaya kuhudhuria mazishi,” amesema Bw Kagwe.
Waziri Kagwe pia amewaonya wazazi wenye watoto wachanga akiwahimiza wawe waangalifu zaidi kwa sababu “maradhi haya hayachagui umri.”
“Kati ya visa vilivyoripotiwa leo (Alhamisi) kuna mtoto mwenye umri wa miezi sita na kwa hiyo ni muhimu kwa wazazi kuwa waangalifu sana hasa kwa kukaa nyumbani,” ameongeza waziri Kagwe.
Idadi ya waliopona imefika watu 375 baada ya tisa wa hivi punde kuruhusiwa kuondoka hospitalini.
Idadi ya wahanga walioangamia kwa sababu ya Covid-19 nchini ni watu 50.