COVID-19: Familia zaidi ya 25,000 Nairobi zapokea msaada wa serikali
Na SAMMY WAWERU
SERIKALI inaendelea kusambaza msaada wa pesa kwa familia zisizojiweza katika baadhi ya mitaa na hasa ya mabanda jijini Nairobi.
Kamishna wa Nairobi Wilson Njenga amesema Alhamisi kwamba jumla ya familia 25,629 zimepokea msaada huo kupitia mfumo wa kutuma pesa kwa simu.
Kwenye kikao na wanahabari Nairobi, Bw Njenga amesema kila familia inapokea Sh1,000 kwa wiki kununua chakula.
“Idadi hiyo ya familia inafika watu 382,033,” kamishna huyo akasema.
Serikali imekuwa ikikosolewa kwa kupuuza familia zisizojiweza, na ambazo zinaendelea kuhangaika kukosa chakula athari za Covid-19 zikihangaisha wananchi.
“Tunafutilia mbali tetesi zinazoenea eti hatusambazii watu chakula. Tunawatumia pesa wanunue chakula,” Bw Njenga akaambia wanahabari.
Kamishna huyo aidha amewataka wasamaria wema pamoja na mashirika, wanaojitolea kusambaza vyakula na bidhaa zingine za kimsingi kwa watu wasiojiweza, kushirikisha serikali katika shughuli hiyo.
Kamishna Njenga alisema kushirikisha maafisa wa serikali, ikiwamo idara ya polisi, kutasaidia kuepusha msongamano wa watu kama ilivyoshuhudiwa eneo la Kibra, tukio alilosema linaenda kinyume na taratibu na sheria za Wizara ya Afya kuzuia msambao wa virusi vya corona.
Watu kupoteza ajira, biashara, hoteli na baadhi ya kampuni na mashirika kufungwa, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa chakula, ni miongoni mwa athari za Covid – 19, ugonjwa ambao umekuwa kero kote ulimwenguni.