• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
BURUDANI: Ana vibao kemkem vya kuzindua, asubiri mawimbi ya Covid-19 yatulie

BURUDANI: Ana vibao kemkem vya kuzindua, asubiri mawimbi ya Covid-19 yatulie

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

JANGA la corona ndilo limemchelewesha kurudi nyumbani kutoka Dubai kuzindua vibao kemkem ambavyo angali ana uhakika vitaitikiwa vizuri na mashabiki wa muziki wa sasa na wa karne mpya.

Elpina Monje almaarufu Elpy Monje anasema ameandaa vibao kemkem ambavyo alikuwa na nia ya kuvitoa mwezi huu Mei, lakini anasubiri corona imalizike ili arudi nyumbani kutoka Dubai anakofanya kazi.

Elpy Monje ni mwanamuziki wa Pwani anayeinukia kwa kasi na anasubiri kwa hamu arudi nchini ili mashabiki wote wa muziki wafurahie zawadi kutoka kwake; nyimbo.

“Nimetayarisha vibao kadhaa ambavyo ningependa kuvivizindua kwetu Kenya. Nasubiri kwa hamu janga tul’o nalo kwa sasa likome; nirudi nyumbani ambako nitafanya mipango ya kutayarisha tafrija maalum ambayo nitawaalika wanamuziki wenzangu,” Monje akasema.

Msanii huyo akiwasiliana na mwandishi huyu kwa njia ya simu alisema ni vile yuko kazini huko ndilo jambo linalomfanya asubiri kuzindua kibao chake kipya ambacho hakupenda kukitaja jina lake hadi atakapofika nyumbani.

“Nina imani na uhakika kibao changu hicho kitaweza kuwapendeza kwa kila aina ya madaha kwani sina shaka hata wanamuzikki wenzangu watakifurahikia,” akasema Monje; msanii mpole na mwenye kupenda kutabasamu wakati wote.

Anasema mafanikio yake katika fani ya muziki yametokana na radhi za wazazi ambazo anaamini ndizo zinazomsaidia pakubwa kuinukia vizuri na kutambulika kuwa mwanamuziki mwenye kutamba na kupata umaarufu wa haraka.

Elpina Monje almaarufu Elpy Monje. Picha/ Hisani

“Mara tu nilipoamua kuwa mwanamuziki, wazazi wangu walinipa radhi kwani walitambua katika fani hiyo sidhamirii kujiingiza kwenye anasa ama mambo mengine mabaya. Nawaomba wazazi wengine waige mfano huo kwani muziki wakati huu ni ajira tosha inayoweza kutusaidia sisi wanawake kuinua uchumi wetu,” akasema Elpy Monje.

Mpango wake mwingine anaotaka kuutekeleza anaporudi nchini kutoka Dubai, anaazimia kufanya mipango ya kwenda nchi jirani ya Tanzania ambako anatarajia kutafuta msanii aliyebobea afanye kolabo naye.

“Nimekuwa nawasiliana na mmoja wa waimbaji mashuhuri wa huko TZ na nina matumaini makubwa nikirudi, nitapata fursa ya kuimba naye,” akasema Elpy ambaye huko Dubai anakofanya biashara, amewahi kuimba.

Elpy Monje amepata umaarufu kwa kibao chake cha ‘I Love My Babe’ ambacho kimepokelewa vizuri na mashabiki wa muziki hasa kwenye mtandao wa YouTube na mitaani kote nchini na hasa katika eneo la Pwani.

Anasema alitambua kuwa na talanta ya kuimba tangu shuleni Taita Taveta ambapo alikuwa miongoni mwa wale walioshiriki kwenye Tamasha za Muziki.

Wimbo wake wa kwanza ulikuwa ‘Nakuwaza’ ambao aliurekodi huko Dubai mwaka 2017.

You can share this post!

Luis Enrique afananisha soka bila mashabiki uwanjani na...

Mwendwa kikaangioni kuhusu mamilioni ya Afcon 2019

adminleo