• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
MWANAMUME KAMILI: Kichwa kisicho akili hata kikinolewa ni kazi bure tu!

MWANAMUME KAMILI: Kichwa kisicho akili hata kikinolewa ni kazi bure tu!

Na DKT CHARLES OBENE

KILA masika na mbu wake! Ndivyo walivyosema wahenga.

Haya masika ya corona yamekuja na zilizala ya “TikTok!” Ndiyo kero ya sasa inayomumunya muda wote ambao tungetumia kubadili mazingira ya jamii, mawazo ya watoto na maisha yetu.

Ndio udhia unaotufyonza tukabaki magofu tu ya watu wasiojua hadhi ya mwanamume kutumia vyema muda aliojaaliwa. Ama kweli akili zisizopata hazina pato. Kichwa kisicho akili hata kikinolewa ni bure tu.

Eti tumeanza huu mchezo wa kuvuana na kuvishana nguo – mke za kiume na mume za kike! Kunani sasa?

Muda wote tuliopewa kufanyia kazi nyumbani, tumeuharibu kupakia na kupakua vijikanda vya “TikTok!” Hebu tuondoe huu mzaha na tutafakari kwa kina jinsi jamii ingenufaikia nguvu na muda huu tunaotema ovyo kama mate. Mwanamume sharti kuwa mwanamume kamili. Huu mchezo wa “TikTok” hauna nafasi katika maisha ya mja mwenye akili.

Sielewi vipi binadamu aliyetunukiwa akili razini anavyoweza kuamua mwenyewe kuzuzuka na kufanyia maisha mzaha! Hivi leo binafsi ninadhikika moyoni si haba kukumbuka muda wote wa ujanani nilioutematema kufanya mzaha. Ninajuta, tena sana, kutowajibikia wote waliohitaji uwezo, akili na nguvu zangu. Ninajuta kuchelewa kuafikia malengo yangu binafsi. Ningalitumia muda wangu vyema ningalikuwa mbali sana. Ningalikuwa karibu mkabala na thurea za nyota angani.

Sihadaike ewe mume mwenye kupenda na kupendezwa mno na mzaha maishani. Katika hii dunia ya “kulambatia vitanga” hakuna mke ataolewa na mwanamume jina. Mnaweza kucheza densi kwenye kanda za “TikTok” shibe yenu. Lakini mwisho wa siku, mla minofu ni mwingine! Unaweza kumfaa na kumtononesha janajike lakini mchinjaji ni mwingine. Kama michezo ndiyo mapenzi, basi tuwape shela vimwana wa leo. Wanajua ya kujua, wanafanya ya kufanya. Haidhuru. Mtakuja kumbuka mapera msimu wa maembe umekwisha!

Mwajua tena jinsi mapenzi yanavyoweza kuwalevya nyie mnaosisimkia ngozi na minofu ya majike. Mtakuja tambua wazi kwamba mapenzi ya dhati hayana muda wa mbwembwe za “tik tok!” Mwanamume huna nyumba, huna mali, huna jina, huna mbele! Kwa unyonge huu hata malimali hailiki haitafuniki! Hakuna mapenzi ya dhati kati ya hawa vichuna wa leo na majuha nyie mnaobahatisha maisha kwenye vijumba tuta. Hata mende wanaozuru kwangu kutafuta chajio afadhali! Hilo litie kibindoni!

Huu muda tunaoharibu kunakili kanda za “TikTok” unatosha watoto kuwakwamua angalau kuwajuza hisabati na isimu jamii. Si nyinyi majivuno mliosoma na kufuzu vyuoni? Si nyinyi mnaotetemesha mashavu kila siku kulaani hali duni ya walimu na elimu yao katika shule zetu? Hivi leo, kuna watoto hawajaona hata ukurasa wa kitabu tangu shule kufungwa. Kuna wengine wanaotazama tu picha na nambari kwenye mabuku lakini hakuna wanachokielewa. Hawa ndio wangekuwa “TikTok” yetu.

Kila siku tunapovuka midomoni kuteta na kutetea “shahada zetu zinazoozea nyumbani”. Sasa tudhihiri hizo akili zetu kwa kuwapa watoto masomo angalau kuwanoa makali kabla hawajarejea shuleni. Ndani ya huu muda tuliozuiliwa na watoto nyumbani, mbona hatujabadili fikira zao angalau wakaona maana ya kuzaliwa kutoka nyonga zetu?

Nawahurumia sana hawa watoto waliotoka katika nyonga zenu nyie mliozama mitandaoni badala ya kuwafaa maishani. Hakuna mtoto ataona wema wala kufurahia mzazi asiye chembe cha akili angalau kufanya jambo la maana maishani. Mnaweza tumia muda huu kucheka na kuchekacheka kama wendawazimu lakini majuto ni mjukuu huja baadaye. Wanaume kwa wanawake wa leo ni sawa na corona. Ni majanga tu!

Huu muda ulitosha vilevile kupanda mboga na matunda kondeni angalau tusijelalia mate kila siku. Ulitosha kusafisha miji na vijiji kuondoa majitaka! Ulitosha kupiga deki nyumba zetu angalau kuondoa utandabui kutani. Muda ulitosha kujifunza mapishi na kuwafunza watoto wetu.

Tangu serikali kote duniani kuamuru kwamba “wananchi wazuiliwe nyumbani ili kudhibiti janga la corona” kumeibuka mazuzu ya watu wanaokesha na kuamkia mitandaoni kupakua na kupakia kanda za “TikTok!” Kweli ulevi hauhitaji mvinyo tu. Huu ni ulevi usioweza kumlisha wala kumvisha mtu. Wanawake kwa wanaume kubadilishana nguo kisha kupakia kanda hizo mitandaoni sio kazi wala bazi inayoweza kumfaa mtu na wanawe!

Siku zote nilidhani wanadamu wanahitaji tu muda ili kufanikisha maisha yao. La hasha! Hata tukipewa miaka na mikaka, akina sisi tutasalia papa hapa tukilalamikia serikali kwa kukataa kutupa masurufu, unga na sukari. Sasa nasadiki kwamba tumekuwa wanaume wanaofikiria kutoka tumboni badala ya akilini. Mende kufia mekoni ni mapenzi yake.

 

[email protected]

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Nahitaji mpenzi lakini nahofia kuchezewa...

MUTUA: Iweje sasa Rais Trump anawatetea Waafrika?

adminleo