UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Aina mbili za ukweli wa kisanaa katika Fasihi
Na ALEX NGURE
MWANADAMU ndiye muumba wa kazi ya fasihi na yeye ndiye aiwasilishaye kazi hiyo ya fasihi; na yeye ndiye anayeishi maisha ya kuathiri na kuathiriwa.
Fasihi kwa hivyo inahusu hali hii ya taathira baina ya mwanadamu na mazingira yake na mwanadamu na mwanadamu mwenzake katika maisha yao.
Maudhui ni kipengele muhimu katika fasihi. Lakini kipengele hiki cha maana hakina budi kuambatana na ukweli.
Mwanafasihi mashuhuri Leo Tolstoy, amelizungumzia sana jambo hili la ukweli wa kisanaa katika insha zake za Nini Sanaa? Katika kazi hii, Tolstoy anazungumzia aina mbili za ukweli wa kisanaa:
Kwanza, anasisitiza kuwa si lazima kila aliloliwasilisha au alilolizungumzia mwandishi kuwa linaweza kutokea. Mwandishi ana uhuru wa kusisitiza mambo ambayo hayapo, kwa dhamira ya kusisitiza kwamba, kama yangalikuwepo ulimwengu ungefana.
Hivyo mwandishi, kwa mujibu wa Tolstoy, anaweza kushughulikia tamani, laiti, au ndoto. Katika nathari ya Kiswahili kuna mifano kadhaa ambapo mwandishi huweza akaumba umbo la kisanaa kusisitiza dhana fulani ambapo anajikita kwa kutamani, huku akielewa kuwa ukweli wa dhana hiyo hauyamkiniki.
Mifano
Tuchukue mifano michache. Katika ‘Kurwa na Doto’, M. S. Farsi anasisitiza usamehevu. ‘Kama mtu mathalan, amekuibia chako k.v. mchumba, mkeo, au mumeo, umsamehe na umpange urafiki. Labda hili analosisitiza Farsi ni jambo zuri, lakini katika maisha ya kawaida jambo hili liko mbali sana na ukweli wa mambo.
Katika ‘Adili na Nduguze’ ya Shaaban Robert, usamehevu umekuzwa zaidi. Humo, tunaambiwa kwamba hata kama mtu, zaidi ya mara moja, akijaribu kukuangamiza au kukuua, msamehe. Jambo hili ni gumu kutokea katika uhalisi wa mambo hata kwa walokole!
Katika riwaya ya Shaaban Robert, ‘Kusadikika’, kuna usamehevu ambao unapatikana pamoja na utetezi na uzalendo wa hali ya juu wa Karama. Ule ujasiri wa Karama, ingawa ni mzuri, unatuachia alama ya kuuliza kama tutautia katika kipimo cha hali halisi.
Wa aidha, waandishi tuliowataja hapo juu walielewa fika kwamba, maelezo yao na visa wanavyovisimulia na matendo ya wahusika wao; picha wanazozichora na matukio wanayoyajenga, yanatoka nje ya mstari wa ukweli na mantiki; ila kwa madhumuni fulani, hasa ya kusisitiza wema. Hivyo, iliwabidi kutia chumvi kazi zao. Mbinu hii kwa mujibu wa Tolstoy, inakubalika kisanaa-ingawa mtu angekuwa na maoni mengine kuhusu njia za kufikia wema, utu na usafi wa tabia kuliko njia zilizopendekezwa na waandishi tuliowataja.
Vitabu vingine vilivyotiwa chumvi kiasi cha kuonekana kazi za kinjozi ni ‘Kufikirika’, ‘Utu Bora Mkulima’ na ‘Siku ya Watenzi Wote’ vya Shaaban Robert. Vingine ni ‘Mtu ni Utu’ cha George A. Mhina na hata katika riwaya ya kileo kama vile ‘Nagona’ ya Euphrase Kezilahabi.
Katika msisitizo wa maudhui kwa mwelekeo wa kutia chumvi, tunapata utanzu wa fasihi simulizi, mathalan: visaasili, kharafa, ngano, mighani n.k.
Uhalisia
Ukweli wa pili, ambao Tolstoy ameusisitiza ni ule wa kueleza mambo kama yalivyo; yaani ile hali ya mwandishi kueleza matendo kama vile yeye mwenyewe angeweza kutenda kama angekuwa katika hali hiyo. Je, kwa mfano, mwandishi angeweza kulala nyumba moja na mwendawazimu anayehujumu watu? Je, mwandishi angeweza kujirusha kutoka ghorofa ya ishirini na kuweza kufika chini salama? Je, mwandishi angeweza kukabiliana na simba watatu na kupigana nao na kuwashinda?
Kama mwandishi asingeweza kuyatenda haya, haifai kuwalazimisha wahusika wake kutenda mambo asiyoyaweza yeye mwenyewe. Na kama atawalazimisha wahusika wake kutenda hayo, basi hisia anazotaka kuziibua kwa wasomaji wake hazitaibuka; kwani yeye mwenyewe haamini hayo wala hana hisia nayo.
Hali hii ya mwandishi kupima ukweli wa mambo ni njia ya kupima hisia na ukubalifu wa wasomaji pia. Ni vizuri mwandishi kujichovya kwa hisia kwenye matendo anayoyaandikia aone kwamba yangaliweza kumfuma na kumsadikisha msomaji wake.
Afanyavyo hivyo, kazi yake itakuwa na taathira kubwa: kama ni kuchekesha itachekesha, kama ni kuogofya itaogofya, kama ni kuliwaza italiwaza, kama ni kuliza italiza. Labda hii ni siri ya mwandishi kumteka msomaji. Ni siri ya kudhibiti hisia za msomaji kiasi kwamba akiaza kukisoma kitabu, hatakiweka chini hadi amalize kukisoma.