Habari

Uhuru atawaweka hadi 2022?

May 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

MASWALI yameibuka iwapo Rais Uhuru Kenyatta atafaulu kudumisha usemi wake katika chama cha Jubilee kuelekea 2022, kwa kubuni miungano na vigogo mbalimbali wa kisiasa.

Tashwishi hizo pia zimezungumziwa ikiwa Rais atafaulu kuendelea na kasi ya mabadiliko ya sasa, ambayo wengi wamefasiri kuwa yanalenga kumtenga Naibu Rais William Ruto.

Kulingana na wadadisi, hofu hiyo inatokana na historia ya kutodumu kwa miungano ya kisiasa nchini tangu mwanzoni mwa mfumo wa utawala wa vyama vingi vya kisiasa 1992.

Rais Kenyatta amepanua mbawa zake kisiasa na kukumbatia viongozi wenye ushawishi nchini, kwenye hatua ambayo duru zinasema inalenga kumng’oa mamlakani Dkt Ruto kupitia hoja ya kutokuwa na imani kwenye Bunge la Kitaifa.

Tayari, Rais amebuni mkataba wa kisiasa na Seneta Gideon Moi (Baringo), aliye pia kiongozi wa Kanu.

Mkataba huo ushawasilishwa kwa Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, ndiye aliyekuwa kiongozi wa kwanza kisiasa nchini kuanza kushirikiana na Rais Kenyatta kupitia handisheki mnamo Machi 2018. Zaidi ya hayo, kinara wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, pia ameeleza nia yake ya kutaka kubuni ushirikiano sawia na Rais Kenyatta.

Kiongozi mwingine ambaye pia ameripotiwa kujumuishwa kwenye mpango huo ni Bw Isaac Ruto, ambaye ni kiongozi wa Chama Cha Mashinani (CCM). Bw Ruto alihudumu kama Gavana wa Bomet kati ya 2013 na 2017.

Lakini licha ya hatua hiyo, wadadisi wanasema hata kama Rais Kenyatta atafanikiwa kubuni muungano huo na kuwashirikisha wanasiasa hao serikalini, mtihani mkuu utakuwa kuudumisha na kutimiza matakwa yao hadi 2022.

Kulingana na Bw Charles Mulila ambaye ni mchanganuzi wa siasa, huenda wanasiasa wakaanza kutoa masharti yao ya kujumuishwa kwenye serikali, hali ambayo inaweza kumlazimu Rais Kenyatta kubuni nyadhifa ambazo hazitambuliwi kikatiba.

Mdadisi huyo pia anarejelea historia ya miungano ya kisiasa nchini, akisema haidumu hata kidogo, kwani huwa inasambaratika mara tu baada ya wanasiasa kutimiza malengo yao.

“Tumeshuhudia miungano mingi ya siasa nchini tangu 1990, wakati Wakenya walianza kumshinikiza Rais Mstaafu Daniel Moi kurejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa. Muungano wa kwanza ulikuwa wa chama cha FORD (Forum for the Restoration of Democracy). Huu ulikuwa ni muungano ulioonekana kuwapa matumaini wanaharakati wengi waliokuwa wakipigania mfumo wa demokrasia ya vyama vingi,” asema Bw Mulila.

Kulingana naye, uwepo wa viongozi wakuu kama Jaramogi Oginga Odinga, Kenneth Matiba, Charles Rubia kati ya viongozi wengine ulizua taswira ya muungano ambao ungedumu kwa kuiondoa Kanu mamlakani.

Wadadisi wanaeleza kuwa huenda isishangaze kwa baadhi ya wanasiasa kuondoka serikalini, ikiwa matakwa yao hayatatimizwa na kubuni muungano na Dkt Ruto, iwapo atang’olewa mamlakani.

Ikizingatiwa kuwa wanasiasa kama Dkt Ruto na Bw Odinga washawahi kuwa pamoja katika ODM, wadadisi wanaeleza kuwa hakuna lisilowezekana katika siasa, kwani wote wanaongozwa na nia ya kufanikikisha maslahi yao.