Makala

KIPWANI: Ana kiu ya kufanya kolabo na wasanii wa haiba ya juu

May 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KAMA wanavyopenda wasanii wengine wanaoinukia, naye pia ana kiu na hamu ya kufanya kolabo na wasanii wenye majina makubwa.

Hivyo ndivyo alivyo msanii wa Mtwapa, Irene Njeri almaarufu Queen Renee aliye na hamu ya kupata fursa ya kuimba na mwimbaji wa Bongo mwenye sifa kote barani Afrika, Diamond Platnumz kwani anaamini kuimba naye kunaweza kumfanya apate umaarufu wa haraka.

“Nina imani kubwa nikipata fursa ya kuimba na mmojawapo wa waimbaji wa Wasafi na hasa mwenyewe Diamond, umaarufu wangu utapanda kwa kasi,” anasema Renee.

Queen Renee ni mwimbaji kutoka mji wa Mtwapa, Kaunti ya Kilifi ambaye umaarufu wake umetokana na nyimbo zake za ‘Champagne’, ‘Kuchikuchi’ na ‘Jiachie’ ambazo kwa wakati huu zinaendelea kutamba kwenye stesheni za redio na televisheni pamoja na mtandao wa YouTube.

Renee anasema mwaka uliomalizika wa 2019 umekuwa wa mafanikio makubwa kwake ingawa ametoa vibao vichache. Nyimbo alizoimba mwaka uliopita ni ‘Tulia tulia’, ‘Shake it’ na ‘Mario’ na zote tatu zimeitikiwa vizuri.

“Siku chache zijazo ninatarajia kuzindua kibao kipya cha ‘Umeninasa’ na kingine ‘Long time’ ambacho ninafanya kolabo na mwimbaji Gunda Weche, Mkenya anayeishi Uswisi,” akasema.

Kumhusu huyu mwimbaji Weche, Renee anasema hajawahi kukutana naye ila alimtumia vocals na yeye huku nchini akarekodi. Hivi karibuni, anatarajia kuzindua wimbo mpya wa ‘Umenigusa’.

Kuhusu shoo, Renee anasema mwaka 2019 alifanya shoo nne pekee kwa sababu alitumia muda mwingi kusoma lugha.

“Nilitumia muda fulani wa mwaka uliopita kwa kusoma lugha na ndio maana sikuweza kufanya shoo nyingi,” akasema.

Renee anasema kuwa muziki wa Kenya unakubalika ila wanamuziki wanahitajika kupewa nafasi na vyombo vya habari na hasa redio na televisheni kuwaangazia. Pia anasema ni muhimu kwa wanamuziki wa Pwani wawe ni wenye kujituma.

Msanii wa Mtwapa, Irene Njeri almaarufu Queen Renee. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Analalamika kuwa Pwani, wasanii wa kike huwa hawapewi shoo kubwa zinazofanyika mjini Mombasa.

“Huwa tunasahaulika hata mtu anaweza kudhani kuwa hapa eneo la Pwani hatuna wasanii wa kike,” akalalama Renee.

Anazitaja baadhi ya shoo ambazo huwa waimbaji wa kike hawatambuliwi kwamba ni ile ya Safaricom ambayo ilifanyika PrideInn Hotel na nyingine ni ile iliyofanyika Mama Ngina Drive siku ya Mashujaa Dei ambayo Renee anasema alikuwako lakini hakukuwa na msanii yeyote wa kike jukwaani.

Hivi sasa wewe unajichukulia kuwa msanii uliye na kiwango gani hasa cha muziki?

RENEE: Ninajihisi kuwa nimeanza kuwa mwanamuziki wa kutambulika sio hapa Pwani pekee bali hata sehemu nyingine za nchi na zaidi jijini Nairobi ambapo nimekuwa nikiimba kwenye kumbi za starehe ukiwemo ule wa Dolce The Club ambapo nilialikwa mara mbili.

Muziki wako zaidi ni wa mitindo gani? Je, huwa unapenda kuimba muziki wa nje wa mtindo wa Bongo Fleva, kama walivyo wanamuziki wengi hapa nchini?

RENEE: Mimi huwa sina mtindo maalum bali naimba kwa kutumia mitindo mbalimbali lakini zaidi ni ule wa Afro Pop. Sijatoa wimbo wowote wa mtindo wa Bongo Fleva, lakini naona hivi karibuni nitatoa kibao kimoja kwa sababu wapenzi wa muziki wangu wameniomba nifanye hivyo.

Kumekuwa na fununu nyingi kuwa nyinyi wanamuziki wa kike huwa munajiingiza kwenye mapenzi hasa munapofanya kolabo na waimbaji wanaume. Je, wewe umewahi kufikiwa na hilo?

RENEE: Hilo linategemea na msanii wa kike mwenyewe alivyo. Kwangu kamwe haliko hilo lakini siwezi kukanusha kuwa wako waimbaji wa kike ambao ni wenyewe wanapenda kujiingiza kwenye mapenzi sio kwa waimbaji wenzao pekee bali hata wanapokwenda kuonana na maprodusa. Wengine hata mavazi wanayovaa yanakuwa ya kumjulisha produsa kuwa nini anachohitaji; si kuimba pekee!