Landilodi ang'oa paa la nyumba ya dereva anayeugua Makongeni
Na LAWRENCE ONGARO
FAMILIA moja katika mtaa wa Makongeni, Thika imeachwa kwa baridi baada ya landilodi kung’oa paa la nyumba yao.
Aliyekomboa nyumba hiyo ni Bw Patrick Mwaura ambaye alikuwa dereva wa matatu lakini anaugua na hawezi kufanya kazi.
Mkewe dereva huyo anasema ya kwamba landilodi alifika hapo wiki moja iliyopita na kung’oa mabati ya nyumba yao kwa kukosa kulipa kodi ya Mei 2020.
Kulingana na mama huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake, mumewe amekuwa mgonjwa kwa mwezi mmoja sasa ambapo yeye ndiye anayeshughulika kumnunulia dawa.
“Mimi huwa nafulia watu nguo mitaani lakini tangu homa ya corona ivamie nchi, nimekosa kibarua hicho,” akasema mama huyo.
Alisema kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa amepitia masaibu mengi kwa sababu mumewe anaendelea kuugua na pia analisha watoto wanne.
“Maisha kwa sasa yamekuwa magumu hata ninatoa mwito kwa wahisani wajitokeze ili wanisaidie nilishe familia yangu,” akasema mama huyo aliyeonekana kusononeka.
Alitoa nambari ya simu ya mumewe ambayo ni 0701 233938 ili wahisani wajitolee kumsaidia kwa chochote walicho nacho.
Alitoa mwito kwa serikali izungumze na malandilodi popote walipo wawe na utu badala ya kuwafurusha wapangaji kama wahuni.
“Wakati huu wa Covid-19 mambo ni magumu kwa kila mwananchi na kwa hivyo wajue masaibu haya yatakwisha,” alisema mama huyo.
Anawaomba wasamaria wema wajaribu kumsaidia ili aweze kumnunulia mumewe dawa ambaye anazidi kulemewa na ugonjwa.
Alisema maisha yamekuwa magumu kwa sababu mvua inayonyesha inawanyeshea kila mara.
Anaiomba serikali kuingilia kati ili kuokoa familia yake ambayo imeachwa katika hali ngumu ya maisha.