Habari Mseto

Waliopona Covid-19 nchini waongezeka

May 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANDISHI WETU

IDADI ya waliopona ugonjwa wa Covid-19 nchini ilifika 402 Jumatatu baada ya watu wengine tisa kuthibitishwa kupata nafuu.

Nayo idadi ya waliofariki hapa Kenya kutokana na maradhi hayo yaliyogundulika mara ya kwanza China mwaka 2019 ilifikia 52 kufuatia kuaga dunia kwa mmoja wa wagonjwa.

Akitoa takwimu za kila siku kuhusu maradhi hayo, waziri msaidizi katika Wizara ya Afya Dkt Mercy Mwangangi alitangaza kuongezeka kwa maambukizi hadi 1,286 baada ya watu wengine 72 kuthibitishwa kuambukizwa.

Takwimu hizi zilitokana na watu 2,711 kufanyiwa vipimo huku jumla ya watu waliofanyiwa vipimo vya Covid-19 nchini tangu Machi ikiwa 61,971.

Hii ina maana kuwa idadi ya waliothibitishwa kuugua virusi vya corona nchini ni asilimia mbili ya walifanyiwa vipimo.

Dkt Mwangangi alieleza kwamba miongoni mwa visa hivyo vipya, 52 ni kutoka Nairobi, 11 kutoka Mombasa na saba kutoka Kiambu.

Kaunti za Isiolo na Turkana ziliripoti kisa kimoja kimoja.

Miongoni mwa visa hivyo vipya 72, watu 70 walitambulishwa kama Wakenya huku hao wengine wawili wakiwa raia wa Uganda na Somalia.

Dkt Mwangangi aliwahimiza Wakenya kuendelea kuzingatia masharti ya Wizara ya Afya akisisitiza kwamba hali bado si shwari.

Katika hatua walizopiga, Dkt Mwangangi alisema kuwa ingawa hali ilipoibuka kulikuwa na maabara mbili pekee nchini za kupima virusi hivyo, kwa sasa kuna zaidi ya 20 katika maeneo tofauti nchini.

Pia alisema kuwa kufikia sasa wametoa mafunzo kwa wahudumu 11,000 wa afya na wahudumu wa kijamii 60,000 katika kaunti zote 47, pamoja na kuwa na vituo vya karantini vyenye nafasi za watu 5,000.