• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
GOZI LA VIDUME: Borussia Dortmund yaalika Bayern Munich

GOZI LA VIDUME: Borussia Dortmund yaalika Bayern Munich

Na MASHIRIKA

MUNICH, Ujerumani

VITA vya ubabe kati ya chipukizi Erling Braut Haaland na kigogo Robert Lewandowski vitatarajiwa kutawala leo Jumanne uwanjani Signal Iduna Park nyota hao wawili watakapokutana kwa mara ya kwanza katika gozi la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Haaland ambaye ni mzawa wa Norway ataongoza safu ya mbele ya Dortmund huku Lewandowski ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Poland akitazamiwa kuwa tegemeo la Bayern Munich ambao kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 61, nne zaidi kuliko Dortmund ambao ni wa pili.

Mabao 10 ya hadi kufikia sasa ambayo yamefungwa na Haaland katika Bundesliga yamesaidia Dortmund kutia kapuni jumla ya alama 27 kutokana na mechi 10 zilizopita mwaka 2020.

Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 19 alicheka na nyavu katika ushindi wa 4-0 uliosajiliwa na Dortmund dhidi ya Schalke wiki moja iliyopita.

Ingawa hakufunga goli katika mchuano wa wikendi uliowakutanisha na Wolfsburg, Haaland alichangia mabao yote mawili yaliyofumwa wavuni na Achraf Hakimi na Raphael Guerreiro katika ushindi huo wa 2-0.

Ambacho kinamwaminisha zaidi kocha Lucien Favre wa Dortmund kwamba kikosi chake kitazamisha chombo cha Bayern ni ushirikiano mkubwa kati ya Haaland na kiungo mvamizi Jadon Sancho atakayepangwa leo Jumanne katika kikosi cha kwanza cha Dortmund baada ya kusazwa benchi dhidi ya Wolfsburg.

Hamasa zaidi kwa mkufunzi Favre ni kupona kwa beki Mats Hummels aliyewahi kushindia Bayern mataji matatu ya Bundesliga kabla ya kurejea Dortmund mnamo Julai 2019.

Hummels anatazamiwa kushirikiana vilivyo na Emre Can atakayejaza nafasi ya Mahmoud Dahoud na Axel Witsel atakayewajibishwa katika nafasi ya Thomas Delaney kwenye safu ya ulinzi.

Dortmund wataendelea kukosa huduma za nahodha wao Marco Reus ambaye amekuwa akiuguza jeraha la goti tangu Februari 2020.

You can share this post!

Wanawake wanne waacha watoto wao katika hospitali Thika

SHINA LA UHAI: Covid-19 tishio kwa sekta ya afya duniani

adminleo