Covid-19: Visa vingine 72 vyaripotiwa
NA FAUSTINE NGILA
Watu wengine 72 wamethibitishwa kuwa na virusi vya corona huku idadi kamili ikifika 1,286 Jumatatu.
Waziri msaidizi katika Wizara ya Afya Dr Mercy Mwangangi alisema visa hivyo vilipatikana baada ya kupima sampuli 2,711.
“Kati ya hao 72, watu 44 ni wanaume na 28 wanawake na umri wao ni kati ya miaka 12 na 78. Mtu mmoja zaidi ameaga dunia, waliofariki kutokana na Covid-19 sasa ni 52,” alisema alipohutubia wanahabari jijini Nairobi.
Nairobi inaongoza kwa visa vingi Jumatatu, baada ya watu 52 kuthibitishwa kuugua, ikifuatwa na Mombasa kwa watu 11 na Kiambu watu 7.
Kaunti ya Isiolo imerekodi kisa kimoja, nayo Kaunti ya Turkana imerekodi kisa cha kwanza eneo la Kakuma huku virusi hivyo vikiendelea kuenea nchini ambapo jumla ya kaunti 29 sasa zimeripoti visa vya Covid-19.
Mitaa ya Nairobi iliyorekodi visa Jumatatu ni Lang’ata kwa visa 21, Dagoretti Kaskazini 15, Kamukunji 4, Kibra 4, Embakasi 2, Kasarani 3. Dagoretti Kusini, Makadara na Mathare zimekuwa na kisa kimoja kila mtaa.
“Katika eneo la Mombasa, visa vinne vimeripotiwa Nyali, Mvita 3 na Changamwe kimoja. Visa saba vya Kiambu vimeripotiwa maeneo ya Limuru, Githunguri, Kabete, Ruiru, Thika na Kikuyu.
Mkurungezi Mkuu wa Afya Patrick Amoth alisema kwamba madaktari 34 wamepatikana na virusi vya corona, lakini sio wote walipata virusi hivi kazini.