Huenda mzozo wa karo shuleni Makini ukatatuliwa kortini
NA OUMA WANZALA
Mzozo kati ya wazazi na usimamizi wa shule ya msingi ya Makini kuhusiana na karo ya muhula wa pili na masomo ya mitandaoni umezidi huku uwezekano wa suala hilo kufikishwa kortini ukishamiri.
Kamati ya wazazi na walimu inayoogonzwa na Nixon Bugo imekataa mahitaji ya karo yaliotolewa na mwenye shule anayesisitiza kwamba lazima wazazi walipe karo.
Barua iliyoandikiwa wazazi na kamati ya wazazi na walimu Mei 22 ilisema kwamba wazazi hawapaswi kulipa karo yeyote kwani serikali haijataja ni lini shule zitafunguliwa.
Advtech walikuwa wamewaandikiia barua Mei 20 huku wakisema kwamba masomo ya mitandaoni si ya bure na hayawezi kuwa ya bure.
Kamati hiyo inakejeli barua hiyo na kusema masomo ya mitandaoni yanafaa kutolewa bila malipo.
“Usimamizi wa shule unaendelea kuwalipisha wazazi kinyume na sheria kwa muhula wa pili ilhali Wizara ya Elimu haijatoa tarehe za muhula huo. Hii inaonyesha ukosefu wa uaminifu, na ukweli kwa upande wao. Usimamizi huo unaendelea kutojali matakwa yanayotolewa na wazazi,” ilisema barua iliyoandikwa na kamati hiyo.
Hata hivo, usimamizi wa Makini unasisitiza kwamba kamati hiyo aina uwezo wa kuamua kitu chochote kinachohusu jinsi shule itakavyoendeshwa.
Migogoro kati ya wazazi na shule za kibinafsi imepanda kutokana na masomo ya mitandaoni huku shule zikibakia kufungwa.