Habari Mseto

Washukiwa wawili wa mauaji ya twiga kushtakiwa leo Garissa

May 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na FARHIYA HUSSEIN

WASHUKIWA wawili ambao inadaiwa walimuua twiga kisha kuuza nyama yake katika Kaunti ya Garissa wamekamatwa.

Akithibitisha tukio hilo, afisa wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini (KWS), Pascal Magiri alisema kuwa wanaume hao wawili walikamatwa katika eneo la Dubandubusa, Masalani eneo la Ijara.

“Walikuwa kwenye pikipiki ambayo walikuwa wakitumia kuleta nyama ya twiga jijini labda kwa kuuza au matumizi ya nyumbani,” alisema.

Washukiwa hao walikuwa na silaha kama panga ambayo ilikuwa imejaa damu.

Hata hivyo, mmoja aliyekuwa akiendesha pikipiki alitoweka.

“Wawili hao watapelekwa mahakamani ili wawe funzo kwa wengine ambao wanaua wanyamapori na kuwauza karibu na eneo hili,” akasema Bw Wagiri.

Aliwapongeza wakazi kwa kufanya kazi kwa karibu na KWS na akawasihi wasifiche majina yoyote ya wanaoua wanyamapori.

“Wanyama wa porini hawako salama tena. Tunawarai nyote mjitolee na kuwa macho. Ikiwa utaona kitu chochote cha kutilia shaka tujulishe,” alisema.

Wawili hao wanatarajiwa kushitakiwa katika mahakama ya Garissa leo Jumanne.

Machi 2020 jamii ya Ijara iliamka na kuapata mifupa ya twiga wa kike mweupe na ndama wake baada ya kuuawa na majangili.

Twiga huyo alikuwa kama shine ya utalii katika hifadhi ya Ishaqbini Hirola.

“Mauaji yake yalikuwa pigo kwa watu wa Ijara. Alikuwa twiga wa kipekee ambaye alivutia wanasayansi na watalii ulimwenguni,” alisema meneja wa hifadhi hiyo Mohammed Ahmednoor