• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Natembeya ‘apiga marufuku’ wanasiasa kuzuru Narok

Natembeya ‘apiga marufuku’ wanasiasa kuzuru Narok

Na SAMMY WAWERU

KUFUATIA mzozo wa kijamii unaoendelea katika Kaunti ya Narok, Mshirikishi wa eneo la Bonde la Ufa George Natembeya amepiga marufuku ziara za wanasiasa eneo hilo.

Kwenye kikao na wanahabari mjini Nakuru, Bw Natembeya amesema Jumanne kwamba aghalabu “wanasiasa hawana jukumu lolote katika eneo hilo kwa sasa.”

“Tunawapiga marufuku wanasiasa kutembea kuliko na mzozo,” amesema mratibu huyo.

Mnamo Jumamosi jioni, mzozo wa kijamii ulizuka katika kijiji cha Oloruasi, kaunti ndogo ya Narok Kusini, ukitokana na wizi wa mifugo.

Jumapili na Jumatatu, maafisa wa usalama walikabiliwa na kipindi kigumu kutuliza ghasia baina ya jamii mbili zinazoishi eneo hilo, zilizokuwa zikizozana.

Watu wawili wamethibitishwa kuuawa, kufuatia mzozano huo wa kijamii.

Bw Natembeya amesema hakuna silaha zozote zitakazokubalika kumilikiwa na wakazi.

“Tumekubaliana hakuna silaha humo, hakuna mishale wala nyuta. Bunduki zilizo mikononi mwa wakazi zinatafutwa,” amesema.

Ili kuzima ghasia, mshirikishi huyo amesema hali ya usalama imeimarishwa ambapo maafisa zaidi, wanaojumuisha wa kukabiliana na ghasia, GSU na wale wa kukabiliana na wizi wa mifugo, wameongezwa kushika doria.

Kuleta maridhiano, Natembeya amesema Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) itashirikishwa katika mazungumzo yatakayoandaliwa baina ya wawakilishi wa jamii zinazozozana.

Mwaka 2018 katika eneo lilo hilo, mzozo wa aina hiyo baina ya jamii hizo ulishuhudiwa na kusababisha vifo vya watu si chini ya wanne.

You can share this post!

KURUNZI YA PWANI: Wakazi wahimizwa wajiandae hali ya...

Pigo kwa AC Milan mkongwe Zlatan Ibrahimovic akipata jeraha

adminleo