• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
WASIA: Geuza changamoto inayokukabili iwe daraja la ufanisi wako wa kesho

WASIA: Geuza changamoto inayokukabili iwe daraja la ufanisi wako wa kesho

Na HENRY MOKUA

UNAPOMWONA Angelica Hale akiimba, unashawishika kufikiri kwamba ni mtoto aliyelelewa kwa tunu na tamasha, bila changamoto zilizo kawaida kwa watoto.

Mwimbaji huyu mchanga aliyeibuka wa pili katika shindano la America’s Got Talent mnamo mwaka wa 2017 huvutia kweli na kuwateka wote wanaomtazama na kumsikiliza.

Upekee wa mshawasha na raghba yake anapoimba huwa msingi wa wengi kutaka kujua ni kipi kinachomtuma vile. Ni baada ya kusaka kiini cha hamasa yake ndipo wengi humaka kugundua kwamba alinusurika kifo katika umri wa miaka minne kutokana na maradhi ya figo.

Ujasiri na ushujaa wa mama yake kumpa mojawapo ya figo zake ili aendelee kuishi ndilo jambo la msingi linalomfanya ajitolee na kuimba kwa mihemko kila apatapo fursa kana kwamba anaimba kwa mara ya mwisho.

Kama sarafu, maisha daima yana pande mbili; upande mmoja mtamu, mwingine mchungu. Fasiri tunayoupa upande wowote uwao ama hutunusuru au kututimba.

Aghalabu maisha yanapotunyooshea shubiri sisi hulaani kila tukio linalozunguka au kuzungukwa na ugumu wenyewe.

Katika baadhi ya miktadha, huwa tunalaani hata kuwa hai kwetu. Lakini je, ni kila shari huwa shari kamili? La, heri nusu shari kuliko shari kamili! Hivi ndivyo twapaswa kuyaona maisha; yaani hali ngumu zinazotukabili zaweza kuwa mbaya zaidi ila tushukuru zinapofikia zifikiapo!

Msimu huu wa corona umesababisha mengi ambayo hatukuyatazamia hata chembe. Huenda mzazi au mwangalizi wako amepoteza kazi au biashara yake kuporomoka. Kama tokeo la hali hii, hata kupata mahitaji ya kimsingi imekuwa changamoto zaidi ya changamoto.

Inawezekana ulitegemea sana msaada wa mwalimu kulimudu somo fulani na sasa haiwezekani kutokana na hali iliyopo. Yamkini nyumba yenu imebomolewa katika ubomozi unaoendelea au imesombwa na mafuriko.

Kila unapotazama nyuma unaona hakurudiki. Mbele nako hakuelekei kuendeka. Unasalia ukisaka majibu ambayo huyapati na badala yake yanazaa maswali zaidi.

Mtazamo

Kuna habari njema kwako! Ukiipa mtazamo unaostahiki, changamoto yoyote inayokukabili leo itageuka kivuko cha kukufikisha mbali kuliko ulivyowahi kufikiri.

Kupoteza kazi kwa mzazi wako huenda ni njia ya kuwatanabahisha kama aila kwamba ipo mibadala mingine ya kipato mliyoipuuza hadi sasa na mwapaswa kuikumbatia.

Kusalia nyumbani na kukosa msaada wa mwalimu huja kumekusudiwa kukusaidia ugundue kwamba waweza kujifunza vyema zaidi kibinafsi kuliko kumtegemea mwalimu daima.

Kuvurugwa na labda kuharibiwa kwa makao yenu kwaweza kuwa msingi wa kukuzindua ewe unayejitapa kwamba wazazi wako wana hiki na kile ukajirekebisha na kulenga kujitafutia mali ya kwako mwenyewe. Wapo waliogundua hili na sasa wanaipongeza corona japo kwa matao ya chini kwa kuwapa fursa hii aali.

Naomba ujitulize na kujiuliza: kipindi hiki cha corona kimeyaathiri vipi maisha yangu kwa njia ninazoziwazia kuwa hasi? Je ni kweli athari hizo ni hasi mia fil mia au waweza kuona tija fulani unapoigeuza changamoto yenyewe na kutazama upande wayo wa pili?

Sikiliza, mashujaa tunaosoma kuwahusu katika Vitabu Vitakatifu na Historia wanatambuliwa kuwa mashujaa kutokana na jitihada zao za kukabili hali ngumu zilizowakumba. Bidii na stahamala zao ndio msingi wa ushujaa wanaotunukiwa!

Wewe pia tambua kwamba kuna awamu ya kuona njozi na ya kuamka ili kuziwania njozi zenyewe. Kuna awamu ya kulia na awamu ya kujifuta machozi, kujituliza na kufanya yanayokujuzu hadi nyota yako ya rehema ing’ae kwako; kwa wema au shari! Fanya jambo la pekee litakalokukumbusha hali ngumu unayoipitia kwa sasa pindi corona iwapo historia. Kila la heri!

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Ubora wa mtu daima huwa ni mtu mwenyewe

NDIVYO SIVYO: Kiima kinapodhibiti upatanisho, sentensi...

adminleo