• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
SIHA NA LISHE: Karafuu na faida zake

SIHA NA LISHE: Karafuu na faida zake

Na MARGARET MAINA

[email protected]

PEMBA, Visiwani Zanzibar, Tanzania inasifika sana kwa uzalishaji wa karafuu.

Zao hili kutoka kwa mkarafuu lina matumizi mengi, ambapo hutumika kama kiungo katika vyakula na vinywaji, dawa kwa maradhi ya tumbo, meno na misuli.

Vilevile karafuu hutumika katika kuleta harufu nzuri ya kinywa, mwili na mazingira pale nyumbani.

Mafuta ya karafuu hutumika kusugua misuli inayouma, kutengeneza dawa za meno na manukato.

Karafuu hutumika kwenye vyakula mbalimbali ikiwemo nyama, biriani, pilau, mchuzi, biskuti na katika chai na maziwa.

Karafuu husaidia usagaji mzuri wa chakula tumboni na ni nzuri ikitumika kutibu maumivu ya tumbo, tumbo kujaa gesi na kiungulia.

Inapotumika katika viwanda kama malighafi ya kutengenezea dawa za meno, hakikisho huwa ni upatikanaji wa bidhaa nzuri ya kutunza meno na kuondosha maumivu ya meno na fizi, kung’arisha meno na kuleta harufu nzuri ya kinywa.

Harufu iliyomo katika karafuu husaidia kuondoa harufu mbaya mdomoni.

Karafuu pia husadia kutibu vidonda vya mdomo na kuimarisha afya ya fizi pamoja na kuzuia meno kuoza.

Karafuu inatumika katika urembo

Wanawake hupenda kusugulia mwili (scrub) kwa kuchanganya unga wa karafuu kavu iliyosagwa na mafuta ya nazi na liwa ambapo husuguliwa mwili mzima kwa ajili ya kuondoa uchafu na kuufanya mwili kuwa mwororo. Liwa ni rojo ya mliwa na sandali inayotumika kama dawa ya joto la ngozi au manukato.

Sabuni zinazotengenezwa kwa karafuu huondoa vipele na chunusi na hivyo kuifanya ngozi iwe nyororo na yenye kuvutia.

Mafuta ya karafuu husaidia matatizo katika mfumo wa upumuaji, kusafisha koo na hutibu kikohozi, mafua, na pumu.

You can share this post!

Wanasoka wa KPL kupokea Sh10,000 kila mmoja kila mwezi...

AFYA: Manufaa ya juisi ya mua

adminleo