Kindiki, Murkomen, Cherargei wakataa nafasi mpya walizopewa katika seneti
Na CHARLES WASONGA
SENETA wa Tharaka-Nithi Kithure Kindiki amekataa nafasi mpya aliyoteuliwa kuhudumu kama mwanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Haki, Sheria na Haki za Kibinadamu.
Kwenye taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari Jumatano jioni, Profesa Kindiki aliyeng’olewa kutoka wadhifa wa Naibu Spika wa Seneti Ijumaa wiki jana, amesema sasa anataka kuelekeza juhudi zake katika kuwahudumia Wakenya kama Seneta wa Tharaka-Nithi.
Amesema hana haja na jukumu hilo jipya ambalo alifahamu kulihusu kupitia kwa vyombo vya habari.
“Kwa heshima nakataa nafasi hiyo. Kuanzia sasa, ninataka kuelekeza juhudi za kuwahudumia watu wa Tharaka-Nithi na Wakenya kwa ujumla kama Seneta,” akasema Profesa Kindiki.
Hatua yake inafuatia ile ya wenzake, Kipchumba Murkomen na Samson Cherargei ambao walikataa nafasi mpya walizopewa baada ya kuondolewa kutoka nyadhifa walizoshikilia hapo awali.
Katika mabadiliko yaliyotangazwa na kiranja wa wengi katika seneti Irungu Kang’ata, Profesa Kindiki aliteuliwa mwanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Haki, Sheria na Haki za Kibinadamu kuchukua nafasi ya Bw Cherargei aliyepokonywa nafasi hiyo. Hiyo ina maana kuwa Seneta huyo wa Nandi pia alipoteza wadhifa wa mwenyekiti wa kamati hiyo, cheo ambacho ameshikilia kuanzia 2017.
Naye Bw Murkomen ambaye aliong’olewa kutoka wadhifa wa kiongozi wa wengi aliteuliwa mwanachama wa Kamati ya Ugatuzi kuchukua nafasi ya mwenzake wa Laikipia John Kinyua aliyetimuliwa kutoka kamati hiyo.
Bw Kinyua amekuwa akihudumu kama mwenyekiti wa kamati hiyo tangu 2017.
Naye Bw Cherargei alikataa nafasi mpya ya kuwa mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Mamlaka na Hadhi ya Bunge la Seneti. Angechukua nafasi ya Bw Kang’ata ambaye alipandishwa cheo na kuwa kiranja wa wengi.
Mwandani mwingine wa Naibu Rais William Ruto aliyepoteza katika mabadiliko hayo ni Seneta wa Meru Mithika Linturi. Alipoteza nafasi yake ya mwanachama na naibu mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Haki, Sheria na Haki za Kibinadamu.
Vilevile, Bw Linturi alipoteza nafasi yake nyingine kama mwanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu na Uwekezaji (CPAIC).
Maseneta hawa wanne waliadhibiwa na chama cha Jubilee kwa madai kuwa walikiuka misimamo na maamuzi ya chama hicho.
Kwa mfano, Mbw Murkomen, Cherargei na Kinyua walikaidi amri ya Bw Kang’ata kwamba waunge mkono hoja ya kumwondoa mamlakani Profesa Kindiki, kama naibu spika.
Seneta Linturi aliteuliwa kuwa mwanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Sheria Mbadala (Committee on Delegate Legislation).
Seneta wa Bomet Christopher Langat pia hakusazwa kwa kupinga hoja ya kumtimua Profesa Kindiki. Mhadhiri huyo wa zamani katika Chuo Kikuu cha Egerton alipoteza wadhifa wake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Elimu.