Habari

Rais Kenyatta asisitiza hatafanya kazi na watu wanaohujumu ajenda zake

May 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amekariri kuwa hatafanya kazi na watu wenye nia ya kuyumbusha ajenda za kufanikisha maendeleo ambazo ameazimia kutekeleza chini ya utawala wake.

Kwenye mahojiano na Mkurugenzi wa Uhariri wa Shirika la Habari la Nation Media Group (NMG) yaliyopeperushwa Jumatano jioni kupitia runinga ya NTV, Kiongozi wa Taifa alisema hawezi kufanya kazi na watu ambao wamepofushwa na ndoto zao za kuingia mamlakani siku za usoni badala ya kumsaidia kufanikisha ajenda yake ya maendeleo kwa raia.

Japo hakumtaja mtu kwa jina.

“Usiruhusu ndoto zako kuhusu mambo ya kesho kuvuruga yale ambayo unapaswa kufanya leo. Kile ambacho unafanya leo ndicho kitakufanya upate kile ambacho unataka kesho. Ni hayo tu na ninayaelewa hivyo,” akasema.

Rais Kenyatta alisema hayo huku mkutano wa Baraza la Kitaifa wa Baraza Kuu (NEC) wa Jubilee ukitarajiwa siku chache zijazo kuidhinisha kutimuliwa kwa wandani wa Naibu Rais Dkt William Ruto kutoka nyadhifa za uongozi katika Bunge la Kitaifa.

Kauli yake pia inajiri siku chache baada ya wandani wengine wa Ruto kung’olewa kutoka nyadhifa za uongozi katika Seneti.

Wao ni maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Susan Kihika (Nakuru) na Kithure Kindiki (Tharaka-Nithi) ambao walipokonywa nyadhifa za kiongozi wa wengi, kiranja wa wengi na naibu spika, mtawalia.

Katika mahojiano hayo, Rais Kenyatta alisema mchakato wa kuwaondoa wabunge na maseneta waasi kwa chama cha Jubilee unalenga kukinga ajenda zake.

“Nataka kufanyakazi na watu ambao hawatapiga vita ajenda ya maendeleo ambayo niliwaahidi Wakenya. Nataka watu ambao wataunga mkono ajenda hiyo,”akasema.

Rais Kenyatta ambaye pia ndiye Kiongozi wa Jubilee alisema amebakisha muda mfupi zaidi kabla ya kuondoka mamlakani na hivyo, “sitatumia muda wangu kuwabembeleza watu fulani.”

“Kwa hivyo, ikiwa unahisi kwamba huwezi kuunga mkono ajenda yangu, mbona usiniruhusu kuweka mtu mwingine ambaye ana ari na umakini wa kunisaidia kufanikisha ajenda hiyo?” Rais Kenyatta akahoji.

Alisema hana chuki na mtu yeyote na kwamba mabadiliko yanayoendelea sasa yatawapa nafasi wale ambao wanataka kuendelea kuchapa siasa kufanya hivyo.

“Nafasi hizi ni muhimu kwangu katika jitihada zangu za kufanikisha ajenda zangu. Kwa hivyo, ni heri niweke mtu ambaye yuko tayari kutumia wakati wake na nguvu kuniwezesha nifaulu,” Rais Kenyatta akasema.

Kiongozi wa taifa akasema pia ushirikiano wake na kiongozi wa upinzani Raila Odinga na vyama vingine unalenga kuunganisha nchini.

“Sijawafikia viongozi wengine kuharibu yale ambayo tumefikia. Nafanya hivyo ili kuendeleza yale ambayo tayari tunayo,” akasema Rais Kenyatta.

Alioenekana kuashiria kuwa ajenda ya mpango wa maridhiano (BBI) ilisitishwa kwa muda tu na janga la Covid-19 lakini mpango huo utarejelewa hali ya kawaida ikirejea.

Rais Kenyatta alisema anashangaa ni kwa nini baadhi ya watu wanaingiza siasa katika mchakato wa BBI.

“Huu mpango unalenga kuondoa hali ya kutoelewana kwa kuhimiza maelewano miongoni mwa Wakenya wa tabaka mbalimbali,” akasema.