Habari Mseto

Sodo za bei nafuu kwa mabinti wa jamii za chini

April 25th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na VALENTINE OBARA

WASICHANA na wanawake kutoka jamii zenye mapato ya chini wanatarajiwa kunufaika na sodo ya bei nafuu iliyozinduliwa na kampuni ya P&G.

Kampuni hiyo inayotengeneza sodo za Always ilizindua aina mpya ya Always Cotton Soft ambayo itauzwa kwa Sh50 kila pakiti yenye sodo nane, tofauti na Sh80 ambayo huwa bei ya wastani.

Hatua hii pia inatazamwa kama mbinu ya kujitafutia soko kutoka kwa ushindani wa sodo za bei ya chini zinazoagizwa kutoka nchi za kigeni kama vile Uchina.

Meneja wa bidhaa hiyo, Bi Ivy Kimani, alisema kampuni hiyo inalenga kuboresha hali ya maisha kwa wasichana na wanawake wanaotoka katika jamii zenye mapato ya chini, ambao hupata hasara za kibiashara au kimasomo kila wakati wanapoenda hedhi kwa kukosa uwezo wa kununua sodo.

“Sasa watapata bidhaa bora kwa bei nafuu ambayo itawawezesha kuendeleza maisha yao kama kawaida,” akasema.

Suala la kuwezesha wasichana na wanawake kupata sodo kwa njia rahisi ni miongoni mwa yale yanayoshinikizwa kimataifa kuleta usawa wa kijinsia kwa kuwapa wanawake uwezo zaidi maishani.

Bi Kimani alisema uwezo wa wanawake wengi huathiriwa na wanapoenda hedhi na hali hii huwasababishia umaskini.