Walemavu zaidi ya 800 wapokea chakula Thika Magharibi
Na LAWRENCE ONGARO
SERIKALI itaendelea kuwajali walemavu na wasiojiweza kimaisha hasa kipindi hiki kigumu ambapo dunia inakabiliana na janga la Covid-19, amesema kamishna.
Naibu kamishna wa Thika Bw Douglas Mutai alisema Alhamisi serikali pia imefanya juhudi kuona ya kwamba inaajiri vijana kazi.
Alisema matokeo ya athari hasi za Covid-19 zimekuwa ni kampuni nyingi kufunga shughuli zao na kuwafuta watu kazi.
Alisema awamu ya kwanza ya kuajiri vijana katika mradi wa kazi kwa vijana imegharimu takribani Sh18 milioni katika eneo la Thika Magharibi.
Bw Jackton Omondi wa kijiji cha Kiandutu anasema baada ya kuajiriwa katika mradi wa serikali wa kazi kwa vijana maisha yake yamebadilika kabisa.
“Sasa ninaweza kupata chakula cha kila siku na hata kusaidia familia kwa jumla. Kwa hivyo, serikali izidi kutupatia nafasi tuendelee na kazi hiyo,” alisema Bw Omondi.
Bi Monica Wairimu kutoka Kiganjo, Thika anasema sasa hategemei wazazi wake kifedha.
“Mimi ndiye nasaidia sasa angalau katika kununua chakula na pia najifanyia mambo yangu bila kuwategemea wazazi,” alisema Bi Wairimu.
Mnamo Alhamisi, walemavu wapatao 898 kutoka Thika Magharibi, walinufaika kwa kupokea chakula ikiwemo mifuko ya unga wa ugali na unga ngano.
Naibu kamishna alisema kwa siku walemavu hao hupokea Sh1,000 huku serikali ikitumia jumla ya Sh3.6m kila wiki.
Alisema hata wazee wa Nyumba Kumi ambao pia hujumuishwa wakati wa kusambaza chakula, watapokea usaidizi.
Alisema wahisani wote wanaotaka kusaidia ama kwa kutoa chakula au msaada mwingine wafanye hivyo kupitia afisi ya naibu kamishna baada ya kuwasiliana na chifu wa eneo husika.
“Hatutaruhusu mtu yeyote kusambaza chakula cha msaada kabla ya kupitia afisi ya serikali,” alisema Bw Mutai.
Alisema wamepata ya kwamba hata waendeshaji wa bodaboda, waendeshaji baiskeli, na wale wa Tuktuk, wanastahili kupokea chakula kwa sababu wengi wameajiriwa.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika, Bw Alfred Wanyoike, alisema kwa miezi miwili sasa biashara nyingi zimesambaratika kabisa.
“Wafanyabiashara wengi wamekwama kabisa ambapo hawana mwelekeo kwa sasa,” alisema Bw Wanyoike.
Alisema kwa sababu wananchi wengi bado wanazidi kugongwa na makali ya njaa, anatoa wito kwa wahisani wazidi kujitolea kusaidia kwa kutoa msaada wa chakula.
Hata hivyo, alitahadharisha wananchi wawe makini na chakula wanachopokea kutoka kwa wahisani kufuatia wakazi kutoka Kikuyu kupokea chakula kilichokuwa na sumu wiki moja iliyopita.