Mawakili walaumu mahakama kwa kupanga kutupa maelfu ya kesi
Na BENSON MATHEKA
MAWAKILI nchini wamelaumu idara ya Mahakama kwa kutisha kutupilia mbali maelfu ya kesi kwa sababu ya walalamishi kukosa kuhudhuria vikao.
Kupitia chama cha wanasheria nchini LSK, mawakili wanadai kwamba hatua hiyo ni dhuluma kwa kuwa Mahakama zimefungwa na huduma zinatolewa kupitia mtandao ambao una changamoto zake.
Mnamo Alhamisi, msajili wa Mahakama Kuu alichapisha ilani akiorodhesha kesi ambazo majaji wanapamga kutupilia mbali kwa sababu ya walalamishi au mawakili wao kuhudhuria vikao.
Kulingana na ilani hiyo, kesi nyingi zilizoorodheshwa ni za mizozo ya urithi, kijamii na mizozo ya biashara.
“Mahakama inawezaje kutoa ilani ya kutupa kesi ilhali haijakuwa ikitoa tarehe za kusikiliza kesi ikitaja janga la corona?” alishangaa mwenyekiti wa LSK Nelson Havi.
Mahakama nchini zimekuwa zikitoa ilani ya vikao vya kesi kupitia mitandao ya kijamii na kwenye tovuti yake.
Hata hivyo, baadhi ya walalamishi wamedai hawapati ilani hizo kutokana na changamoto za mtandao.
“Kuna watu walio sehemu za mashambani ambao hawapati huduma za mtandao. Kutupa kesi zao kipindi hiki cha corona ni kuwadhulumu,” alisema Bw Havi.
Aliomba mahakama inafaa kusubiri mahakama zifunguliwe kabla ya kutupa kesi.
Mawakili wamekuwa wakitaka Mahakama zifunguliwe lakini Jaji Mkuu David Maraga amesema ni lazima maafisa wa mahakama walindwe wakati huu wa janga la corona.
Mawakili wamelaumu Bw Maraga kwa kusukuma majaji wakamilishe kesi kwa vyovyote vile.