FUNGUKA: ‘Hatugusani lakini bado tuna-enjoy’

Na PAULINE ONGAJI

KWA wengi, uhusiano wa kimapenzi unahusisha watu wawili kuishi pamoja na kutumia muda wao mwingi pamoja ili angalau kila mhusika ahisi uwepo wa mwenziwe kwa kumgusa, kumpapasa au hata kumbusu.

Mojawapo ya sababu ambazo zimefanya mahusiano na ndoa nyingi kuvunjika ni wapendanao kuishi au kufanya kazi mbali baina yao.

Lakini kwa Ezra, 43, na Nimo, 45, mambo ni tofauti sana. Kwa wawili hawa, mapenzi yao yanazidi kunoga kutokana na kuwa hawaishi pamoja.

Acha nikupe uhondo zaidi. Ezra ni mfanyabiashara jijini Nairobi ambapo anajihusisha na uuzaji magari na pia ana nyumba kadha za watu kuishi au kufanyia biashara kwa kulipia kodi kila mwisho mwezi.

Nimo ni daktari katika hospitali moja kubwa jijini Nairobi, kazi ambayo ameifanya kwa takriban mwongo mmoja sasa.

Kutokana na taaluma zao, wawili hawa wana pesa na pia wamewekeza katika sekta mbalimbali; kumaanisha kwamba hawana matatizo ya kifedha.

Lakini hii leo hatuzungumzii suala la kifedha kuwahusu, bali penzi na ndoa yao ya kiajabu, kama anavyosimulia Nimo.

“Kwetu, mapenzi sio lazima yawe na mgusano. Tunaishi katika nyumba tofauti ambapo tukitaka kushiriki mahaba, tunafanya hivyo kwa njia ya simu au mtandao wa kijamii.

Kukaa kwetu mbali sio kwamba tunafanya kazi katika miji tofauti. Sote tunaishi Nairobi ila nyumba ni tofauti, suala linalopunguza mgusano wowote.

Tunaweza kukaa hata mwaka mzima bila mmoja kumtia mwenzake machoni, ila tu kwa kuwasiliana kwa simu au mtandao wa kijamii.

Lakini hii haimaanishi kwamba mbinu yetu ya mahaba ni tofauti na ile inayochukuliwa kuwa ya kawaida. Kwa mfano sisi huangaliana kwa macho ya kulegea, tunapapasana kupitia skrini ya simu au kipakatalishi, na hata tunavua nguo. Tofauti ni kwamba hatugusani kamwe.

Ni mbinu inayoridhisha ambapo tukishamaliza kila mmoja anaenda zake kulala, na endapo yeyote atahisi kiu ya kufanya hivyo tena, yuko huru kumpigia mwenzake simu na kuanza tena.

Uzuri wa mbinu yetu ni kwamba mahaba yetu hayatunyimi nafasi ya kila mmoja kutumia muda wake kivyake. Na ikiwa mmoja wetu ana haja ya kuridhishwa kwa mbinu ya kawaida, yuko huru kufanya hivyo, mradi amjulishe mwenzake, na ahakikishe kwamba hatua hiyo haitaathiri ndoa yetu.

Vilevile hatuazimii kuwa na watoto kwani hakuna kujamiiana.

Uhusiano wetu ulianza kama wa kawaida. Tulichumbiana vyema, akaniposa, kunilipia mahari na hata tukafanya harusi. Lakini baada ya muda, ulianza kudorora kutokana na kuishi pamoja ambapo kila mara kulikuwa na ugomvi.

Mara nyingi ugomvi huu ulitokana na uchovu wa kuonana kila mara. Na kutokana na sababu kwamba tulikuwa tunapendana sana na hatukutaka kuuvunja, tukaamua kuzama katika mbinu hii.

Bila shaka jamaa zetu hawafurahii lakini uhusiano ni baina ya watu wawili, na mradi sisi tuna raha, maoni ya wengine hayatubabaishi ng’o!”

Habari zinazohusiana na hii