• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
MWANAMUME KAMILI: Corona katuzidishia dhiki ya majanga ya wanaume!

MWANAMUME KAMILI: Corona katuzidishia dhiki ya majanga ya wanaume!

Na DKT CHARLES OBENE

AFADHALI turejelee hali ya kawaida wanaume kuondoka majogoo na kurudi nyumbani usiku wa manane!

Mwanamume mmoja kanidokezea tabia za jirani mwenye mazoea kusubiri wanawake kwenda bafuni naye akapeleka yake maji na kusimama mlangoni akisubiri zamu yake kuoga! Alikuwa wapi kidudumtu hiki?

Nani katuletea hili janga la corona kutuzidishia “majanga ya wanaume kushinda sebuleni kama makochi?” Tutaepukana vipi tabia za gumegume wanaoelekeza ndewe kudakia yanayofanyika vyumbani kwa majirani? Na wale wenye kutembeatembea kutoka nyumba moja hadi nyingine kutatiza mipango ya “wanaotafuta watoto mchana?” Mwenzako anapasha yake misuli moto, wewe huna haya kwenda “kumtembelea!” Ala! Tembeatembea zako zinamfaidi nini mwenye njaa? Kwani kwako ndiko kusikohitaji “kutembelewa?”

Jamani corona halina budi kurudi kuko huko lilikotoka. Ujaji wanaume nyumbani unazidi tibua amani mitaani. Jamani serikali tufanyie lisilobudi. Tuhurumie akina sisi tunaotaabika tena tunaodhikika kutokana na janga la wanaume wasiojua hadhi ya mwanamume kamili. Mabaa na vilabu kufunguliwa ndio dua zetu! Tunafahamu fika kwamba subirá huvuta heri ila tunakamia mno kuwapa kwaheri gumegume hawa wanaotubughudhi bure. Afadhali wafe kuko huko vilabuni nasi tupate muda kufanya yetu!

Visa vya wanaume kuzozania vijimambo kwenye makazi vimekithiri mno wakati huu wa corona. Kweli, sio tukizi tena kuona wanaume wanachaniana nguo mchana kwenye “ploti!”. Wajua tena dhiki za kuishi kwenye hivi vijumba tuta. Vijumba ambavyo watu wazima kuviziwaviziwa na mabozi wanaopitapita ovyo ni jambo la kawaida ila lachukiza mno. Isitoshe, hivi vijumba vyenyewe havina siri. Watu wazima wanalazimika kujibana ama kujificha kama kwamba ni watoro. Si mwajua tena kuna mambo ya watu wazima yasiojua subira?

Hata “wanaotafuta watoto mchana” wanalazimika kusubiri hadi kiza cha maki angalau kujaribu bahati yao tena. Corona katuzidishia dhiki, kutuletea “janga la wanaume kuketi sebuleni kama viti!” Tatizo ni kwamba wanaume wanaoshinda nyumbani ndio kwanza dhiki kwa wenzao wanaotaka “kujaribu bahati yao!” Vipi? Badala ya kushinda sebuleni kwao, wanatambia ngano na kuchania majani ya miraa kondeni kwa majirani. Presha hiyo siyo? Wengine wanajipa hamnazo kutafuta vimelea kutani na kwenye madirisha ya majirani. Wakakamavu ndio kwanza wanapiga chabo hadharani tu. Ubozi kama huu ndio kwanza unachochea vita vya gumegume kuvaana na kuvuana mitaani.

Jamani wanaume wa leo kunani kuzozana na majirani kila siku? Mbona kufarakana na kupapurana vijijini na mitaani kana kwamba ni wake wenza? Ama ni athari ya kuzubaa nyumbani baada ya mabaa na vilabu kufungwa? Hebu nikariri tena kwa ukakamavu kwamba dunia ya leo haina nafasi wala muda kuvumilia utoto wa baadhi ya wanaume wa leo. Tunahitaji sana watu wanaoona mbele – kwa maana ya kuona mbele! Wala hatuna haja kusikiliza kesi za mitaani zinazohusu wanaume wanaopiga chabo vyumbani kwa majirani wala kukita kutani kwa majirani kudakia yanayoendelea ndani humo. Hatuna budi kusitisha kabisa hizi akili za “vijumba tuta!”

Ujiraini kama ndugu ni kufaana katika mema na mabaya yanayoisukasuka ngalawa ya jamii. Ujirani ni mshikamano unaolenga kuboresha mazingira na hali ya jamii. Ujirani ni karamu na pilkapilka za pamoja tena kwa umoja na ushirika! Ujirani sio kunakili kanda za mapapo na mapigo ya kutani kwa majirani! Wala ujirani sio kukazia macho bafuni wanakokogea vichuna na warembo wake wa majirani.

Mwanamume kamili ni mtu wa haiba na hadhi. Hujulikana hasa kwa unyoofu, utulivu na akili zake razini. Tatizo langu kwa baadhi ya wanaume wa leo ni umakinifu katika maovu na visa vya kitoto. Sidhani kama mwanamume kamili anazo akili za kufia nyufani macho kukazia visivyolika kwa macho. Hivyo sivyo anavyomakinika mwanamume kamili!

 

[email protected]

You can share this post!

Mke wa Rais wa Burundi alazwa katika hospitali nchini Kenya

Serikali yaambia wazazi walipe karo hata kama shule...

adminleo