Makala

TAHARIRI: Tusikubali shinikizo kurejelea soka nchini

May 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

KUMEKUWA na mjadala iwapo mechi za Ligi Kuu (KPL) zinafaa kurejelewa au la baada ya kusitishwa mapema mwezi Machi kutokana na maradhi ya Covid-19.

Baadhi ya wadau katika fani ya soka wanasisitiza kwamba maadamu mataifa ya Ulaya na mengine barani Afrika yametangaza tarehe ya kurejelea ligi zao, Kenya inafaa kufuata mkondo.

Wengine hata hivyo, wanashikilia kwamba msimu huu unafaa kufutiliwa mbali au msimamo wa jedwali la KPL utumiwe kutangaza Gor Mahia kuwa mabingwa wapya.

Kwa mfano, mechi za Ligi Kuu nchini Uingereza (EPL) ambayo inahusudiwa sana nchini zitarejelewa Juni 17, Bundesliga ya Ujerumani ilirejelewa wiki jana, Serie A ya Italia nayo itasakatwa tena kuanzia Juni 20. Barani Afrika, majirani wetu Tanzania wametangaza kwamba mechi za Ligi ya Vodacom zitarejelewa tena kuanzia wikendi ijayo.

Kabla ya kusitishwa kwa muda usiojulikana, timu za KPL zilikuwa zimesalia na mechi tisa au 10 kukamilisha msimu. Swali hata hivyo ni je, tumefikia hali ya kudhibiti virusi vya corona kiasi kwamba tunaweza kurejelea mchezo wa soka na spoti nyinginezo?

Ukweli ni kwamba bado tuna mwendo mrefu kwa sababu idadi ya maambukizi ya corona nchini inaendelea kuongezeka kila wizara ya Afya inapotoa takwimu kila siku. Nchini Uingereza, mikakati mingi ya kuzima maambukizi mapya imewekwa hasa ikizingatiwa kwamba mechi hizo zitasakatwa bila mashabiki.

Wachezaji wanaoshiriki EPL watakuwa wakipimwa virusi vya corona mara mbili kwa wiki, viwanja vyao vitakuwa vikinyunyiziwa dawa ya kuua viini vya corona, wachezaji watakuwa wakisafirishwa kutoka nyumbani hadi viwanjani kwa basi lao kwa pamoja mbali na mikakati mingine.

Ni wazi kwamba hapa nchini hatuna uwezo wa kiuchumi wa kugharimia mikakati kama hiyo kwa timu 17 zinazoshiriki KPL. Timu kama Gor Mahia na AFC Leopards zinakabiliwa na ukosefu wa fedha na haziwezi kugharimia shughuli hiyo ambayo itakuwa vigumu hata kwa serikali kutekeleza.

Aidha, wachezaji wetu hutumia magari ya uchukuzi wa umma na itakuwa kibarua kigumu kuwasafirisha hadi mazoezini na uwanjani siku za mechi. Hatufai kuiga Tanzania au Burundi kwa sababu nchi hizi hazijamakinika katika kuzingatia mikakati ya kuzuia maambukizi zaidi ya Covid-19.