Gavana kujitetea kwa ufujaji wa pesa za kaunti
Na RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA ya Nairobi Ijumaa ilimpata na kesi ya kujibu Gavana wa Busia, Sospeter Ojaamong.
Hakimu Mkuu Douglas Ogoti alisema ushahidi ulionyesha Bw Ojaamong na washukiwa wenzake walifuja Sh8milioni kwa kulipa kampuni moja ya Ujerumani ya kuzoa taka, licha ya kuwa hakuna kazi iliyofanya.
Gavana huyo alishtakiwa mwaka 2019 pamoja na Bernard Yaite, Allan Ekweny na Samuel Ombui.
Wengine ni Timon Otieno, Leonard Wanda, na wakurugenzi wa kampuni hiyo ya Ujerumani ijulikanayo kama Madam R Enterprises, ambao ni Edna Adhiambo, Renish Achieng na Sebastian Hallensleben, raia wa Ujerumani.
Wanane hao sasa watajitetea mbele ya Hakimu Ogoti.
Katika mahakama nyingine, aliyekuwa Mbunge wa Kasarani John Njoroge naye alipatikana na hatia ya kumlaghai kiwete Sh100,000.
Mahakama iliambiwa kuwa Bw Njoroge alipokea hongo kutoka kwa Bw Abdirahman Mohamed Abdullahi aliyekuwa ili aweze kulipwa baada ya kukamilisha ujenzi wa shule katika eneobunge hilo.
Korti iliambiwa kuwa Bw Njoroge alimwambia Bw Abdullahi kwamba malipo yake yangeharakishwa akilipa hongo hiyo mnamo Juni 25, 2013.
“Ni jambo la kuhuzunisha kwamba Njoroge aliamua kudai hongo kutoka kwa kiwete aliyekuwa kwenye kiti cha magurudumu,” Hakimu Mkuu Lawrence Mugambi alisema.