Mtoto umri wa mwezi mmoja miongoni mwa wagonjwa 143 wa Covid-19
SAMMY WAWERU na CHARLES WASONGA
MTOTO mwenye umri wa mwezi mmoja ni miongoni mwa wagonjwa waliothibitishwa Jumamosi Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Rashid Aman alipotoa takwimu za idadi ya maambukizi mapya ya Covid-19 katika kipindi cha saa 24 ambazo zimepita.
Visa vya Covid-19 sasa ni 1,888 baada ya kuthibitishwa vingine 143 baada ya wizara kufanyia vipimo sampuli za watu 2,959 na mgonjwa mwenye umri wa juu ana umri wa miaka 88.
“Wagonjwa wote ni Wakenya ambapo 110 ni wa jinsia ya kiume na 33 ni wa jinsia ya kike,” Dkt Aman amesema.
Dkt Aman amesema mgonjwa mmoja amefariki akiwa na umri wa miaka 53 ambapo idadi ya walioaga dunia nchini kutokana na Covid-19 sasa ikifika watu 63.
Kaunti ya Nairobi na Mombasa, zingali zinaongoza katika maambukizi, Jumamosi Nairobi ikithibitisha maambukizi mapya 88 na Mombasa 25.
Kaunti ya Kericho imekuwa ya hivi punde kuthibitisha maambukizi ya ugonjwa huu baada ya kisa kimoja kuthibitishwa kutoka huko, idadi jumla ya kaunti zilizoathirika sasa ni 33.
Dkt Aman ametangaza kwamba Jumamosi watu 26 wameruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya kupona, idadi jumla ya waliopona Covid-19 sasa ikifika 464.
“Kutokana na visa hivi vipya, sasa idadi jumla ya visa vya maambukizi nchini imetimu 1888,” Dkt Aman amewaambia wanahabari jijini Nairobi, alipokuwa akitoa taarifa ya kila siku kuhusu hali ya janga la Covid-19 nchini Kenya.
Dkt Aman amesema Nairobi na Mombasa bado zinaendelea kuandikisha visa vingi vya maambukizi. Katika mtazampo wa kaunti, Nairobi ina visa vipya 86, Mombasa (25), Uasin Gishu (11), Kiambu (6), Busia (3), Kwale (3), Migori (3), Kajiado (1), Kisii (1), Garissa (1), Isiolo (1), Makueni (1) na Kericho (1).
Katika kaunti ya Nairobi, Makadara inaongoza kwa visa 45, Kibra (21), Embakasi Kusini (6), Kasarani (5), Ruaraka (3), Westlands (2), Embakasi Magharibi (2), Langata (1) Starehe (1).
Waziri huyu msaidizi amewahimiza Wakenya waendelea kufuata masharti yaliyowekwa na serikali kupunguza kuenea kwa maambukizi.